Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika ngazi za elimu

March 6th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

WANAFUNZI wanaelewa vizuri wanapofundishwa katika lugha ya Kiswahili kama anavyosema Brock-Utne (2000) na Brock-Utne (2002).

Vilevile Brock-Utne (2003), anaeleza kwamba lugha zinazotumika kufundishia katika madarasa ya Afrika ni lugha ambazo hazitumiwi na wanafunzi wawapo nje ya shule na wala hawaielewi kwa usahihi.

Isitoshe,  walimu wenyewe hawaitumii lugha hiyo nje ya mazingira ya darasa.

Qorro (2005) anafafanua kwamba Kiswahili ni lugha inayopaswa kutumiwa katika nyanja zote za mawasiliano ya kitaifa hasa katika shule.

Ni lugha inayofahamika vizuri kwa wanafunzi na walimu. Qorro (2005), anaendelea kusisitiza kwamba nchi nyingi duniani ambazo hutumia lugha zake huonyesha mafanikio katika nyanja za uchumi, siasa na jamii.

Mfano mzuri ni taifa la Uchina ambalo ni mojawapo ya mataifa yanaoonyesha mfano mzuri wa kutumia lugha yake kufundishia watu wake na matokeo yake ni kuwa na maendeleo makubwa ya kiuchumi.

Qorro vilevile anabainisha kwamba, Tanzania kuendelea kutumika lugha ya kigeni (Kiingereza) kufundishia elimu ya Sekondari ni dalili ya kushindwa kutumia lugha ya Kiswahili kufundishia elimu ya sekondari, na kusababisha wale wanaotumia lugha hiyo kushindwa kujifungamanisha na wanajamii wenzao.

Balaa kuendeleza mambo ya msingi

Aidha, Qorro anaendelea kudai kwamba,wanafunzi wanapofundishwa kwa lugha wasiyoijua, wanakosa maarifa ya kuendeleza mambo yao ya msingi ya mila na desturi zao, kushindwa kujiamini na kukosa uhuru wa kifikra na kimaarifa, na la kusononesha zaidi kuathiriwa na tamaduni za kigeni zinazoambatana na matokeo ya matumizi ya lugha hizo za kigeni.

Kwa mujibu wa Qorro kama alivyomnukuu Rubagumya (2003), Kiswahili ni lugha inayopaswa kutumiwa katika nyanja zote za mawasiliano ya kitaifa hasa katika taasisi za elimu.

Kutotumika kwa lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu kuna madhara makubwa.

Walimu hushindwa kujieleza vizuri kwa sababu ya kutumia lugha ya Kiingereza ambayo wengi wao hawana umilisi wake wa kutosha na hivyo kusababisha mawasiliano duni baina yao na wanafunzi ambao pia wengi wao hawamudu Kiingereza vizuri.

 

Baruapepe ya Mwandishi: [email protected]

Marejeo

Bryman A. (2008). Social Research Methods.London: Oxford University Press.

Cummins, J. (2008). Teaching for transfer. Challenging the two solitudes assumption in Bilingual education. In J. Cummins & N.H Homberger (Eds), Encyclopedia of Language and Education,2nd Edition,Volume 5. New York: Springer Science + Business Media LLC.

Enon C.J. (1995). Educational Research, Statistics and Measurement. Kampala: Makerere University.