Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya ushairi katika uwasilishaji wa Fasihi

August 9th, 2019 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

USHAIRI wa Kiswahili una dhima kubwa mno katika Fasihi Simulizi na Andishi. Ushairi umetumiwa sana katika tanzu mbalimbali za fasihi kwa sababu mbalimbali.

Nyimbo kwa mfano zimetumiwa sana katika kuandika na kuwasilisha maudhui ya riwaya, tamthilia, novela na hata hadithi fupi.

Zaidi ya mambo mengine, matumizi hayo yana dhima ya kutambulisha wahusika, kujenga tamathali za semi, ishara, taswira, kuweka urari wa vina au mizani na kuonyesha ushiriki wa hadhira katika kazi nyingi za fasihi.

Dhima nyingine ya ushairi katika fasihi ni pamoja na kodokeza, kuibua maudhui na kukuza tanzu za fasihi ya Kiswahili.

Fani

Ushairi una dhima ya kujenga na kuhamisha mbinu mbalimbali za fani.

Hili linathibitishwa na Mugyabuso Mulokozi (2002), anaposema kwamba tabia ya tendi ya kutumia au kuazima mbinu za kifani kutoka katika ushairi wa majigambo huhamisha udokezi na sitiari ambazo hutumiwa sana katika majigambo kwenda kwenye tendi.

Hapa tunaona wazi kwamba pale ushairi wa majigambo unapotumika katika utanzu wa utendi, labda na tanzu nyinginezo za fasihi simulizi, hujenga mbinu za kifani kwa kuhamisha mbinu zile zinazotumika katika ushairi wa majigambo na kuzipeleka katika utanzu husika ambao hutumia ushairi huo wa majigambo.

Zaidi ya kuhamisha sitiari na udokezi, ushairi wa majigambo pia huhamisha chuku na ucheshi, mbinu ambazo hutumika sana katika majigambo.

Vivyo hivyo, nyimbo kama mojawapo ya vipera vya ushairi zinapotumiwa katika riwaya, tamthilia au utanzu mwingine wowote, huhamisha mbinu za kifani zilizopo katika wimbo kwenda katika utanzu husika.

Hadhira

Matumizi ya ushairi katika tanzu nyingine yanasaidia kuibua ushiriki wa hadhira.

Ushiriki wa hadhira ndio msingi wa kazi yoyote ya fasihi simulizi. Sifa hii ni mojawapo ya sifa zinazoifanya fasihi simulizi kuwa hai.

Hivyo, tunaweza kusema kwamba ushairi wa majigambo na ushairi wa Kiswahili kwa ujumla husaidia sana katika kuibua ushiriki wa hadhira katika tanzu nyinginezo za fasihi na hivyo kuzihuisha tanzu husika.

Maudhui

Kazi yoyote ya fasihi hujengwa kwa maudhui na fani.

Maudhui ni jumla ya mawazo yaliyomo katika kazi ya fasihi wakati ambapo fani ni mbinu zitumikazo kwa minajili ya kuwasilisha maudhui hayo.

Ushairi wa Kiswahili unapotumiwa katika tanzu nyinginezo za fasihi, husaidia kuibua au kukazia maudhui yabebwayo na kazi husika.

Kwa mfano, ushairi wa Kiswahili unapotumiwa katika ngano, riwaya, tamthilia au hadithi fupi, husaidia kudokeza maudhui yabebwayo na kazi fulani.

Akifafanua dhima ya nyimbo katika hadithi fupi, Samwel (2012), anaeleza kuwa waandishi wa hadithi fupi huweza pia kutumia nyimbo na hivyo kuonyesha jinsi tanzu zinavyoingiliana, kukamilishana na kutegemeana.

Watunzi wa hadithi fupi hutumia mdokezo wa wimbo ili kuibua maudhui wanaoyakusudia.

Wahusika

Ushairi wa Kiswahili husaidia pia katika kujua kazi husika ya fasihi inatumia wahusika wa aina gani na wenye uwezo upi.

Dhima hii huonekana hasa pale ushairi unapotumika katika utanzu mwingine. Ushairi wa majigambo unapotumika katika tendi, hutambulisha na kujenga sifa mbalimbali za shujaa anayesimuliwa, matendo yake, chakula chake, mavazi yake na mambo muhimu yanayozingira maisha yake.

Vipera

Ushairi pia huweza kukuza tanzu za fasihi.

Inaelezwa na wataalamu mbalimbali kuwa matumizi ya nyimbo pamoja na matumizi ya vipengele vingine vya fasihi simulizi katika fasihi andishi yanakuza vipera vya fasihi hiyo.

Matumizi hayo ya vipengele vya fasihi simulizi ndani ya fasihi andishi ambayo hayakuwapo hapo awali katika fasihi andishi ya Kiswahili, yameibua kile kinachoitwa majaribio katika fasihi na yamezalisha dhana ya ‘fasihi ya majaribio’.

Hivyo, matumizi hayo yameibua riwaya ya majaribio, tamthilia ya majaribio na kadhalika.

Matumizi ya vipera vya fasihi simulizi, ikiwa ni pamoja na ushairi simulizi (nyimbo), yamekuza fasihi andishi ya Kiswahili.

Matumizi hayo ya nyimbo hukazia kwa mfano maudhui yabebwayo na tamthilia husika na kubadilisha mtindo wa uandishi wa kazi hizo.

Aidha, matumizi ya nyimbo hujenga picha, taswira na sitiari katika kazi ya fasihi.

Ushairi wa Kiswahili una dhima kubwa sana katika jamii ya Waswahili na pia kwa fasihi yao na ya jamii nyinginezo.