Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sifa bainifu za wanafunzi wanaojifunza lugha

June 6th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

WAKATI mtaalamu anawafundisha wanafunzi lugha kama Kiswahili, ni muhimu kukumbuka kwamba uteuzi wa njia itakayotumika utategemea aina ya wanafunzi na kazi au majukumu yao.

Sifa za wanafunzi wanaojifunza lugha

Wanafunzi hutofautiana kulingana na tabia zao. Hivyo basi, mwalimu anahitaji kuangalia mielekeo ya wanafunzi wake ili kuwafahamu na kuwaelewa vyema. Baadhi ya tabia za wanafunzi ni kama vile:

· kuna mwanafunzi mwenye hasira za ghafla pasipo kukusudia

· kuna mwenye haya

· kuna mtulivu au mnyamavu

· kuna mcheshi

· kuna mwenye kiburi na asiyepeda kushutumiwa hata akikosea na kadhalika

Athari za kijamii kuhusu lugha na wanalugha

Kila jamii ina mtazamo wake kuhusu shughuli za kujifunza lugha.

Mtazamo hasi ndio ambao huathiri ujifunzaji lugha na kusababisha kukosa mshawasha wa kujifunza lugha. Lugha huathiriwa na mambo kadha wa kadha jinsi yafuatavyo:

· Nia au lengo la kujifunza lugha hiyo – Kwa nini unataka kujifunza lugha hiyo?

· Jinsia; inasemekana wanawake wanaweza kupata lugha kwa urahisi kuliko wanaume.

· Umri; kwa walio na umri mdogo ni rahisi kupata lugha kuliko wenye umri uliopevuka.

· Mazingira; mazingira mazuri yanavutia mwanafunzi kujifunza haraka.

· Umilisi wa lugha kama akiwa na umilisi mdogo

Katika ufundishaji wa lugha ya Kiswahili, mwalimu ana majukumu mahususi anayopaswa kutimiza ili kufanikisha mchakato huu.

Ni sharti mwalimu awape motisha wanafunzi katika kujifunza lugha husika.

Iwapo mwanafunzi anaathiriwa na hasira kwa mfano, ni wajibu wa mwalimu kumsaidia kuondokana na ghadhabu.

Aidha, mwalimu ana jukumu la kuondoa dhana potovu ya ujifunzaji lugha. Kwa mfano, kuna wanaoamini kwamba Kiswahili ni lugha ya Kiislamu.

Mwalimu pia anapaswa kuondoa utata katika vipengele vya kisarufi.

Ni wajibu wa mwalimu kuwaeleza wanafunzi kuhusu aina mbalimbali za lugha na mahali zinapotumika.

Matumizi ya lugha ya ishara ni muhimu sana katika kufahamu ishara zinazotumika katika jamii. Hivyo mwalimu ana wajibu wa kuwaeleza wanafunzi mambo yafuatayo kutegeemea utamaduni wa jamii husika:

. baadhi ya utamaduni huangalia usoni, tabasamu na kujiamini

· matumizi ya mkono wa kushoto au wa kulia

· katika baadhi ya jamii, hairuhusiwi kabisa kuonyesha vidole yaani kumnyooshea mtu kidole

· miondoko ya kusimama na kuelezea jambo

 

Je, umeipenda mada hii? Tuandikie maoni au wasiliana na mwandishi: [email protected]

 

Marejeo

Chiraghdin, S. & Mnyampala, M. (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.

Richards, J.C. (1984). Error Analysis Perspectives on Second Language Acquisition, London: Longman Group Ltd.

Wardhaugh, R. (1986). An Introduction to Socio-Linguistics. New York: Blackwell Publishers.