Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Tathmini ya kina kuhusu Isimu ya Lugha ya Kiswahili

March 19th, 2019 3 min read

Na MARY WANGARI

DHANA ya isimu inaweza kufafanuliwa kama taaluma ya sayansi inayojishughulisha na masuala ya lugha.

Tunaposema kwamba isimu ni sayansi, kuna sifa bainifu zinazodhihirisha kauli hii kama zifuatazo:

Kwanza kabisa kuna hesabu. Isimu hujumuisha hesabu kwa mfano tunapozungumza kuhusu asilimia. Bila shaka hesabu ni somo la sayansi na huitwa takwimu leksika (lexico statistics).

Pili, maneno kutoka kinywani na vile yanavyotoka pamoja na yanakotoka ni tawi la elimu ya viumbe linalojulikana kama Biolojia au Elimu Viumbe.

Biolojia vilevile ni somo mojawapo la Sayansi.

Isitoshe, kuna maabara ya lugha inayotumiwa katika kufanyia lugha uchunguzi hususan katika nchi zilizoendelea sana kama vile mataifa ya bara Uropa.

Jinsi sote tujuavyo, shughuli zinazohusiana na maabara ni za kisayansi. Isimu hutumia mbinu za Kisayansi katika matumizi yake.

Mbinu hizi zinajumuisha uwazi unaotokana na jinsi maneno yalivyopangwa ili kuleta maana iliyo wazi na wala si ya kiholela.

Aidha, katika isimu kuna matumizi ya nguvu au ukipenda msisitizo katika matamshi ya maneno. Matumizi ya nguvu yoyote ile iwe ni katika mwanadamu, mnyama, jua na kadhalika huchunguzwa katika somo la sayansi linalofahamika kama Fizikia.

Katika isimu, kuna ukosefu wa hisia za kibinafsi. Kwa mfano, Isimu Pendekezi (Prescriptive Linguistics) hujitokeza hasa katika lugha mame. Isimu Elekezi (Descriptive Linguistics) hasa hutokea tunapotumia lugha ya pili.

Isimu imeainishwa katika vitengo viwili vikuu ambavyo ni: Isimu pweke na Isimu tumizi. Isimu pweke, hujishughulisha na jinsi sauti za lugha zinavyotamkwa.

Isimu hii nayo imegawanywa katika matawi madogo madogo kama vile fonetiki, fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki.

Isimu tumizi vilevile imegawanywa katika makundi madogo madogo kama vile isimu saikolojia, isimu historia na isimu jamii.
Kwa mintarafu ya makala haya, tutaangazia matawi anuwai ya isimu pweke jinsi ifuatavyo:

Fonetiki

Hiki ni kipengele cha isimu pweke kinachoshughulikia vitamkwa katika lugha. Ni taaluma ambayo hutafiti, huchanganua na kisha kutoa ufafanuzi kuhusu utamkaji na usikivu wa sauti zote kama zinavyoweza kutamkwa katika kinywa cha binadamu, bila kujali iwapo sauti hizo ni za lugha gani. Kipashio cha msingi katika taaluma hii hujulikana kama fonimu.

Fonimu

Hizi ni sauti zinazotokea katika nafasi au mazingira yale yale na kubadili maana aliyokusudia msemaji husika. Kwa mfano, mzungumzaji wa Kiswahili akisikia maneno sindano na shindano yakitamkwa, anang’amua mara moja kuwa maneno hayo yana maana tofauti kabisa.

Ataelewa kuwa sindano ni chombo cha kushonea au kudungia ilhali shindano ni mchuano unaoandaliwa ili kupata mshindi.
Tofauti hii imeletwa na sauti /s/ na /sh/ zinazotokea mwanzoni mwa maneno. Kwa hivyo, katika mfano huu /s/ na /sh/ kila moja ni fonimu.

Alofoni

Hii ni fonimu inayotokea katika mazingira ya kiisimu ya fonimu nyingine bila ya kubadilisha maana. Wakati mwingine sauti zinaweza kubadilisha nafasi lakini bila kubadili maana ya maneno.
Kwa mfano, baadhi ya wazungumzaji wa Kiswahili husema lafiki badala ya rafiki, azabu badala ya adhabu au luga badala ya lugha lakini maana hazibadiliki.

Sauti hizi ni sura mbili za fonimu moja au kwa kutumia neno la kitaalamu zaidi ni alofoni za fonimu moja. Alama za fonimu huonyeshwa katika mistari miwili sambamba, kwa mfano, /t/ huku alofoni zikionyeshwa katika mabano ya mraba mathalan [a]. Fonimu imegawanywa mara mbili yaani irabu na konsonanti.

Fonolojia

Hili ni tawi la kiisimu linalotafiti mpangilio wa sauti na jinsi mpangilio huu unavyoathiri namna maneno yanavyotamkwa katika lugha maalumu. Kipashio cha msingi katika taaluma hii ni fonimu. Mbinu zitumiwazo kujua iwapo kitamkwa fulani ni fonimu katika lugha huitwa jozi-maana (minimal pairs).

Semantiki

Hiki ni kipengele cha isimu kinachoshughulikia maana katika lugha. Ni kipengele kisicho kikongwe sana katika isimu. Semantiki ni kipengele ambacho kimeleta ubishi mkubwa kati ya wanaisimu. Kuna wale wanaodai kuwa katika mofimu kuna maana inayoeleweka.
Kwa mfano neno baba. Japo si sentensi, lina maana. Wengine nao wanadai kuwa maana lazima ipatikane tu katika sentensi kamili. Kwao, neno baba pekee halina maana. Katika semantiki, huwa kuna utata fulani katika sinonimia (synonyme).
Sinonimia ni kundi la maneno tofauti lakini yenye maana moja.
Mifano ya sinonimia:

Binadamu – mtu, mja, adinasi, mwanadamu, mahuluki, insi
Roho – moyo, mtima, fuadi
Marehemu – hayati, maiti, mwendazake.

Kwa uchunguzi wa makini, utaweza kugundua tofauti ya maneno hayo japo ni sinonimia.