Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Udadisi kuhusu sera ya lugha ya kufundishia shuleni barani Afrika

March 27th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

KATIKA shule nyingi za kibinafsi, lugha zinazotumika kufundishia ni za kigeni mathalan Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani na Kiitaliano.

Hata hivyo, baadhi ya mataifa duniani yamedumisha lugha zao na kuzitumia katika sekta ya elimu.

Nchini Japan, lugha inayotumika kufundishia ni Kijapani kwa viwango vyote vya elimu.

Kwa upande mwingine, lugha inayotumika kufundishia katika taifa la Israeli ni Kiebrania huku Kiarabu kikitumika katika shule za waarabu walio wachache.

August na Shanaha (2006) wanasema lugha ya kufundishia nchini Norway ni Kinorwai na Romania lugha ya kufundishia ni Kiromania.

Nchini Urusi vilevile lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu ni Kirusi (August na Shanaha (keshatajwa).

Ni bayana kwamba katika mataifa hayo, lugha za wenyeji ndizo zinazotumika kufundishia shuleni na katika ngazi nyingine za elimu.

Kulingana na Msanjila na wenzake (2000) lugha za jamii ni bora katika kufundishia kuliko zile za kigeni kwa sababu zifuatazo:

  1. Kisaikolojia – lugha ya jamii ni mfumo wa alama zenye maana ambazo katika akili ya mwanafunzi hufanya kazi haraka katika kujieleza na kuelewa.
  2. Kielimu –  Mwanafunzi anajifunza haraka kupitia lugha anayoielewa vyema kuliko kujifunza kupitia lugha ya kigeni.

 

Lugha ya kufundishia katika mataifa mengi barani Afrika ni lugha za ughaibuni kutegemea na mkoloni aliyeitawala nchi husika. Baadhi ya lugha hizo ni Kiingereza (kwa nchi zilizokuwa koloni za Mwingereza),Kifaransa (kwa nchi zilizokuwa koloni la Mfaransa na Mreno) na Kiafrikana katika baadhi ya shule za Afrika Kusini.

Baldauf na Kaplan (2004) wanahoji kwamba katika taifa la Rwanda, Kinyarwanda ndiyo lugha ya kufundishia viwango vyote vya elimu. Naye Molosiwa na wenzake (1991)wanasema kwamba  lugha ya kufundishia nchini Botswana hutumia Kiingereza sambamba na kisetswana ambacho ndiyo lugha ya kwanza kwa asilimia themanini ya wananchi.

Nchini Afrika Kusini, lugha ya Kiingereza hutumika kufundishia shuleni ingawa siku za hivi karibuni katiba ya nchi imetambua lugha nyingine za wenyeji.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Rugemalira, J. M. (2005). Theoretical and Practical Challenges in a Tanzanian English Medium School. Africa and Asia

Senkoro, F. (2004). The role of language in education and poverty alleviation: Tool for access and empowerment in Justian Galabawa and Anders Narman Education poverty and Inequality (eds.) Dar es Salaam: KAD Associates

Skutnabb-Kangas, T. & McCarty, T. L. (2008). Key concepts in bilingual education: Ideological, historical, epistemological and empirical foundations. In J. Cummins and N. H. Hornberger (Eds.), Encyclopedia of Language and Education, 2nd Edition, Volume 5: Bilingual Education. New York: Springer Science + Business Media LLC