Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Udhaifu wa kutumia lugha za kigeni katika kufundishia

March 13th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

TAFITI anuwai zinadhihirisha kwamba lugha za kufundishia shuleni barani Afrika Mashariki zina udhaifu mkuu hususan nchini Tanzania.

Baadhi ya wataalamu waliofanya utafiti kuhusu lugha za kufundishia ni kama wafuatao:

Brock-Utline (2005), katika utafiti wake kuhusu lugha mbili za kufundishia katika madarasa ya shule za sekondari Tanzania, alibainsiha kwamba lugha ya Kiingereza ilikuwa ni lugha ya pili na Kiswahili lugha ya kwanza.

Uchunguzi wake ulibainisha kwamba wanafunzi walielewa zaidi yale maarifa waliofundishwa kwa lugha ya Kiswahili na wakashiriki vizuri katika kutoa michango ya mawazo yao mengi na yaliyokuwa mazuri kinyume cha darasa lilifundishwa kwa Kiingereza.

Kwa upande wa Peterson (2006) wanafunzi wana mawazo chanya kuhusu lugha ya Kiswahili, kwamba wanaelewa zaidi wanapofundishwa katika lugha ya Kiswahili.

Lugha ya Kiswahili wanaitumia nje ya darasa na popote kama sehemu ya maisha yao ya kila siku.

Wanapofundishwa kwa lugha hiyo wanapata maarifa kamili kuliko wanapofundishwa kwa Kiingereza.

Matumizi ya lugha lugha isiyofahamika katika kuwafundishia wanafunzi kunachangia kuzorotesha ubora wa elimu kwa kuwa wanafunzi hawaelewi kile kinachofundishwa.

Naye Mwinsheikhe (2003), katika utafiti wake kwa madhumuni ya kutaka kujua kama kutumia Kiswahili katika mchakato wa kufundisha na kujifunza kunaweza kuimalisha ushiriki na ufaulu wa wanafunzi kwa masomo ya sayansi.

Aligundua kwamba, kuna tatizo la lugha katika kufundisha sayansi.

Idadi kubwa ya walimu walikiri kutumia lugha ya Kiswahili wanapofundisha masomo hayo kinyume na sera ya elimu ya Sekondari.

Aidha, wanafunzi walisema kwamba, wao wanatumia Kiswahili zaidi katika mijadala ya masomo yote ya sayansi.

Mwinsheikhe anahoji kwamba huo woga wa kuamua kutumia Kiswahili unatoka wapi ilhali Tanzania ilishapata kamusi ya mwongozo kwa masomo ya Bayolojia, Kemia na Fizikia tangu mwaka 1990 ambayo inaondoa woga kwa pale palipokuwa na ugumu?

Hivyo basi, kuna uhusiano mkubwa baina ya lugha ya kufundishia na maarifa yanayokusudiwa kupatikana.

Lugha ya kufundishia inatakiwa iwe inayofahamika vizuri kwa wanafunzi na walimu pia.

Aidha, madai hayo yanasawiri taswira kuhusu elimu ya Tanzania ambapo mwanafunzi akiwa shule ya msingi hufundishwa kwa lugha ya Kiswahili na anapohamia sekondari anafundishwa kwa lugha ya Kiingereza.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Rugemalira, J. M. (2005). Theoretical and Practical Challenges in a Tanzanian English Medium School. Africa and Asia

Senkoro, F. (2004). The role of language in education and poverty alleviation: Tool for access and empowerment in Justian Galabawa and Anders Narman Education poverty and Inequality (eds.). Dar es Salaam: KAD Associates

Skutnabb-Kangas, T. & McCarty, T. L. (2008). Key concepts in bilingual education: Ideological, historical, epistemological and empirical foundations. In J. Cummins and N. H. Hornberger (Eds.), Encyclopedia of Language and Education, 2nd Edition, Volume 5: Bilingual Education. New York: Springer Science + Business Media LLC.