Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Ufafanuzi wa wataalam kuhusu dhana ya umilisi wa lugha na isimu

October 8th, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

JINSI tulivyojifahamisha, kuna mbinu nyingi za kukadiria umilisi katika lugha ya Kiswahili au lugha yoyote ile kwa jumla.

Wasomi na wanaisimu anuai wametoa fafanuzi mbalimbali kuhusu dhana ya umilisi wa lugha na isimu., Tutaangazia na kuchambua fafanuzi mbalimbali ili kupata uelewa wa kina kuhusu dhana ya umilisi wa lugha na isimu katika lugha ya Kiswahili katika muktadha wetu.

Kwa mujibu wa msomi Noam Chomsky (1965) ambaye ndiye mwasisi wa dhana ya umilisi wa lugha, umilisi wa lugha ni ule uwezo wa mzungumzaji kuwa na ufahamu fika kuhusu kanuni za kiisimu za lugha anayozungumza.

Kuna kanuni kadhaa muhimu za lugha ambazo kila mwanafunzi wa lugha au mtumiaji yeyote wa lugha anapaswa kuzifahamu ili kuwea kutumia lugha husika ipasavyo.

Kanuni hizo ni pamoja na: Kanuni za kisarufi zinazohusisha fonetiki, fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki pamoja na kanuni za kileksia.

Kando na kuzielewa kanuni hizo, mwanafunzi wa lugha hana budi kujizatiti kufahamu jinsi ya kuzungumza lugha husika ipasavyo hali inayoweza kufanikishwa na kufanya mazoezi mara kwa mara.

Mwanaisimu Newmark (1966) anaonekana kuafikiana na kauli ya Chomsky ambapo anahoji kuwa umilisi wa sheria za kimsingi za lugha, umilisi wa usemaji, umilisi wa isimujamii na mambo mengineyo, ni baadhi ya vipengele ambavyo kila mtu ni sharti ajifahamishe navyo ili kubobea katika umilisi wa lugha.

Kwa upande wake Stern (1983) anafafanua kuwa viwango vya umilisi katika lugha yoyote ile huwa tofauti kulingana msemaji wa lugha hiyo.

Kuwa na kiwango cha juu cha umilisi wa lugha huweza kujitokeza kupitia uwezo wa kuunda maneno na sentensi katika lugha husika. Hapo ndipo mzungumzaji hufahamika kuwa amebobea katika utumiaji au uzungumzaji wa lugha fulani.

Isitoshe, ni sharti mtumiaji wa lugha ni sharti aweze kuitumia lugha inavyofaa katika nyanja nne kuu za lugha ambazo ni pamoja na: kusikiliza, kuzungumza, kuandika na kusoma.

Richard na Rodgers (1986) wanaafikiana na hoja hiyo wakihoji kuwa ili kuwa na kiwango fulani cha lugha hakuhitaji tu umilisi wa kanuni za lugha pekee, bali vilevile uwezo wa kutumia sheria hizo za kiuamilifu yanni katika mazungumzo na maandishi.

[email protected]

Marejeo

Chomsky, N. (1986). Knowledge of language, its nature and use. Cambridge: Mass MIT press.

Newmark, P. (1966), How to interfere with language learning, internal journal of American Linguistics 40.

Stern, H. (1983) Fundamental Concepts of Language Teaching: Oxford; Oxford University Press.