Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Umuhimu wa majaribio, mitihani katika kuimarisha umilisi wa kiisimu kwa wanafunzi

November 4th, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

ILI mwanafunzi aweze kuwa na umilisi wa kiisimu katika lugha ya Kiswahili, ni sharti aambatishe matumizi ya lugha katika usemi na katika maandishi pamoja na kujifahamisha kuhusu kanuni za kisarufi katika lugha ya Kiswahili.

Kwa mujibu wa mwanaisimu Leihman (2006), umilisi wa kiisimu katika lugha yoyote ile huambatanishwa na matumizi yake katika usemi au katika maandishi na kuelewa jinsi lugha hiyo inavyopangwa kisarufi na jinsi inavyoathiri maisha ya mtu.

Aidha, anahoji kuwa umilisi wa kiisimu huhusisha kila kitu kinachohusiana na lugha husika kama vile; mawasiliano, muundo, na utendaji.

Katika mazingira ya shule, majaribio au mitihani huweza kupima umilisi wa mwanafunzi na uwezo wake wa kujibu maswali kwa njia sahihi kwa kutumia lugha ya Kiswahili pasipo walakini wowote.

Isitoshe, umilisi wa kiisimu katika lugha una manufaa katika mazungumzo kwa kuwa humwezesha mtu kuwasiliana na mwenzake kuhusu umilisi wa kiisimu na kuweza kupima umilisi wake.

Mwalimu au mkufunzi anaweza kupima weledi wa mwanafunzi na kiwango chake cha umilisi wa kiisimu kwa kupitia jinsi anavyoandika, anavywasilisha hoja zake kwa mantiki na uwiano kwa kuzingaria kanuni za kisarufi katika lugha ya Kiswahili.

Nadharia ya Umilisi wa Kiisimu wa Lugha ya Lehmann (2006) inajikita katika viambajengo vitatu vikuu ambavyo tutavichambua jinsi ifuatavyo:

Umilisi wa kiisimu hupatikana katika mazoezi na hukua maishani mwa mtu – Kiambajengo hiki hutumika kupima ukuaji wa umilisi wa kiisimu katika maisha ya mtu binafsi.

Kila binadamu huwa na kiwango fulani cha umilisi wa lugha anapoanza kujifunza lugha.

Kiwango hicho cha umilisi wa kiisimu katika lugha husika hubadilika na kuzidi kukua kadri msemaji wa lugha anavyozidi kukua kiumri na vilevile kitaaluma.

Kwa upande wake, Lehmann anahoji kuwa mtu anapozaliwa huanza kufahamu lugha na kadri anavyoendelea kukua ndivyo umilisi wake wa kiisimu huongezeka.

Kwango cha umilisi wa kiisimu katika lugha cha mwanafunzi huweza kupimwa kupitia majaribio maalum ya lugha.

Jinsi tunavyoelewa, mwanafunzi anapojiunga na chuo au shule huimarika kiumri na kimasomo kadri anapoendelea na masomo yake.

marya.wangari@gmail

Marejeo

Lehmann, C. (2006). Linguistic Competence. Erfurt: University of Erfurt.

Massamba, D, Kihore, Y & Hokororo, L . (1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: TUKI ambayo kwa sasa ni TATAKI

Wanyoike, P. (1978), Vikwazo Katika Mafunzo ya Kiswahili Kenya.