Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Utahini wa Karatasi ya Kwanza (KCSE); Insha

April 5th, 2019 3 min read

Na ALEX NGURE

LIFUATALO ni wasilisho la mwalimu Simon Ngige, mwandishi wa Upeo wa Insha, Kiswahili A+ na Kiswahili Encylopaedia, kwenye Kongamano la walimu wa Kiswahili lililofanyika katika Shule ya Upili ya Nakuru tarehe 01/03/2019.

Karatasi ya KCSE – Insha (102/1)

Karatasi hii huwa na maswali manne ambapo mwanafunzi anafaa kujibu maswali mawili pekee.

Swali la kwanza huwa la lazima na huhusu insha za kiuamilifu. Ufuatao ni mfuatano wa maswali yalivyotahiniwa miaka ya awali hadi kufikia mwaka 2018:

1. Barua rasmi (2000)
2. Hotuba -4 (2001, 2005, 2009, 2014)
3. Mazungumzo-2 (1999, 2003)
4. Kumbukumbu-3 (2004, 2012, 2018)
5. Ripoti -4 (1997, 2006, 2015, 2016)
6. Barua kwa mhariri -2 (2007, 2017)
7. Tahariri -1 (2008)
8. Wasifu-1 (2010)
9. Mahojiano -1 (2011)
10. Memo -1 (2013)
*1998 na 2002 hakukuwa na insha ya kiuamilifu


Insha mbazo hazijawahi kutahiniwa:

Risala, Tawasifu, Wasifukazi, Taarifa, Dayolojia, Ilani/onyo/tahadhari/notisi/arafa/faksi, Ratiba, Taarifa/ripoti isiyo rasmi, Baruapepe, makala ya redio/ya televisheni, Shajara na Barua ya kirafiki.

 

Swali la pili aghalabu huhusu masuala ibuka ama huhusu mjadala. Maelezo ya kina ama ufafanuzi wa masuala hayo ni muhimu. Mifano ya masuala ibuka:

Uimarishaji wa usalama, sababu za ajali barabarani na jinsi ya kuzizuia; uteketezaji wa mabweni/migomo shuleni, sababu za wizi wa mitihani, ufaafu wa ugatuzi, matatizo yanayokumba familia/ndoa, matatizo yanayowakumba wanafunzi, madhara ya unywaji wa pombe/utumiaji wa mihadarati, namna ya kuimarisha uchumi wa vijana, namna ya kuboresha mazingira, namna ya kuimarisha jumuia ya Afrika Mashariki, namna ya kuimarisha utangamano wa kitaifa, namna ya kujiandaa kwa mtihani wa kitaifa, namna ya kupambana na ufisadi.

Matarajio ya Ruwaza ya 2030, namna ya kuimarisha michezo, namna ya kukabili ukame/mafuriko, jinsi teknolojia inavyoimarisha maisha, namna ya kupambana na umasikini/ baa la njaa, ufanisi wa elimu bila malipo, uimarishaji wa kilimo, namna ya kupambana na unyanyasaji wa kijinsia, sababu za kuzorota kwa maadili, athari za uwindaji haramu, umuhimu wa miundo-mbinu kama barabara/reli/viwanda, namna ya kuimarisha demokrasia shuleni.

Sababu za kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa, manufaa ya Katiba mpya, umuhimu wa michezo shuleni, utandawazi, kukuza uzalendo, athari za uchukuzi wa bodaboda, nafasi ya vijana katika maendeleo ya nchi, namna ya kuimarisha elimu ya mtoto mvulana/msichana, namna ya kukabili tatizo la chokoraa, namna ya kupambana na ukabila nchini/ vita vya kikabila, namna ya kuimarisha raslimali zetu, namna ya kuimarisha tamaduni zetu, ufanisi wa nchi tangu uhuru.

Namna ya kuimarisha uhusiano kati ya wazazi na wana wao, namna ya kujiandaa kwa mtihani wa kitaifa, changamoto zinazokumba ugatuzi, changamoto zinazokumba wafanyakazi nchini, namna ya kupambana na ugonjwa wa ukimwi,namna ya kuimarisha nafasi za ajira nchini, namna ya kupunguza uhamiaji wa watu kutoka mashambani hadi mijini, na namna ya kuhifadhi misitu yetu.

Methali

Swali la tatu aghalabu huhusu methali – kisa kiwe kimoja tu, kisisimue, kiwe na sehemu mbili, maana ilenge/mtahiniwa aelewe methali kikamilifu, maana ya juu na ya ndani itolewe katika aya ya kwanza/utangulizi, mapambo ya lugha na ubunifu wa hali ya juu.

 

Swali la nne kimsingi huwa insha ya kubuni ama ya mdokezo. Hapa mtahiniwa azingatie maneno ya mdokezo, afasiri maneno hayo kikamilifu, mapambo ya lugha yawepo, kisa kisisimue ajabu, ubunifu wa hali ya juu uzingatiwe, mitindo mbalimbali ya sentensi itumiwe.

Vitahiniwa

Kichwa cha insha

a) Mtahiniwa asiweke kitone au nukta baada ya kichwa cha insha.

b) Kichwa kisipite maneno sita katika insha ya pili na ya nne.

c) Katika insha za kiuamilifu, aghalabu kichwa kitaje aina ya insha inayoshughulikiwa. Kwa mfano, Ripoti kuhusu ukosefu wa usalama nchini, Ilani kuhusu visa vya ufisadi nchini na kadhalika.

d) Katika swali la tatu, andika kichwa cha methali iliyoulizwa. Kwa mfano Haraka haraka haina Baraka. Methali mbadala isitolewe kama kichwa.

e) Katika swali la nne, mtahiniwa atoe kichwa kulingana na swali aliloulizwa. Kwa mfano, Siku ya ajabu maishani mwangu. Asiwe na tabia ya kupachika methali kiholela kama kichwa cha insha yake ya nne. Taharuki iwepo.

f) Kichwa kiwe katika herufi kubwa na kipigiwe mstari mmoja tu

g) Insha zote sharti ziwe na kichwa/vichwa

Baruapepe: [email protected]