Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Utamaduni na lugha ya Kiswahili

September 18th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

KWA mujibu wa msomi Mbaabu (1985), utamaduni unahusu mila, asili, jadi, na desturi za mavazi, vyakula, imani, tabia, na maisha ya jamii kwa jumla.

Anasisitiza vilevile kuwa utamaduni ndiyo msingi wa fasihi.

Katika makala hii, tutajikita katika uchambuzi na upambanuzi wa utamaduni wa Kiswahili ambao bila shaka, ndio kiini cha fasihi ya Kiswahili.

Ni bayana kuwa hatuwezi kutathmini dhana ya utamaduni wa Kiswahili, pasipo kuwaangazia Waswahili nchini Kenya pamoja na kudadisi vipengele kadha muhimu kama vifuatavyo:

Vipengele Muhimu katika Utamaduni wa Kiswahili

1. Uislamu ambao una nafasi ya kipekee katika imani na dini ya Waswahili wengi

2. Malezi ya Kiswahili au ukipenda Uswahili ambayo yanatilia maanani heshima, upole na maadili katika jamii.

3. Mafunzo na vyuo vya Kurani, Maulidi na Kumbini ambazo ni taasisi muhimu katika kuelekeza malezi katika Kiswahili.

4. Kazi mbalimbali za Waswahili ambazo zinajumuisha usafiri wa baharini, uundaji wa vyombo na vifaa vya baharini, uvuvi, ugemaji tembo ya nazi, ukulima, ukwezi, ukuli, biashara na ufundi mbalimbali na kadhalika.

KAZI YA UVUVI KATIKA KISWAHILI

Ni vyema kufahamu kwamba miongoni mwa kazi anuwai za Kiswahili, uvuvi umeangaziwa kwa kina kutokana na uzito wake wa kipekee katika maisha ya Waswahili.

Hii inadhihirika kwa mfano, katika mitego ya samaki ambapo tafiti chungunzima zimefanywa kuhusu mitego anuai inayotumika na nyakati mahsusi zinapotumika.

Hii hasa ni kwa kuwa kazi ya uvuvi katika Uswahili inahusisha vyombo na vifaa mahsusi na hufanyika katika nyakati maalum na hujumuisha itikadi na mbinu mbalimbali.

AINA YA MITEGO INAYOTUMIKA KATIKA KUVUA SAMAKI

Kuna aina sita ya mitego au ala mbalimbali ya kuvulia samaki katika Kiswahili ambayo tutaiorodhesha ifuatavyo:

(i) Aina ya kwanza inajumuisha lasha, sonyi na thasi ambayo ni mitego ya majarifa ambayo aghalabu hutumika nyakati za usiku.

(ii) Pili, kuna mitego inayofahamika kama uzio.

(iii) Aina ya tatu ni nyavu.

(iv) Ni mitego inayofahamika kama shipi.

(v) Mitego inayofahamika kama bunduki. Bunduki hapa ni mshale maalumu wa kupigia samaki baada ya kupiga mbizi majini.

(vi) Huku sita tukiwa na mitego kwa jina kimia.

 

[email protected]

Marejeo

Chiraghdin S. (1974). Kiswahili na Wenyewe. Kiswahili 44:1, kur. 48-53.

Chum H. Utamaduni wa Watu wa Wilaya ya Kusini-Unguja. (Mswada unaotayarishwa kutolewa kitabu, Mhariri Dkt. T.S.Y. Sengo).

Mbaabu I. (Mhar.) (1985). Utamaduni wa Waswahili. Nairobi: Kenya Publishing & Book Marketing Co. Ltd