Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Utaratibu wa somo darasani katika ufundishaji wa lugha ya pili

June 25th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

SOMO lolote darasani linapaswa kuwa na sifa kadha. Sifa zifuatazo ni muhimu sana:

Utangulizi . Unapaswa kutanguliza somo lako; kama sio mara ya kwanza wape chemsha bongo wale wanaojifunza lugha. Kama ni kwa mara ya kwanza, unaweza kuanza na hadithi. Hii itakusaidia kuvuta usikivu wa wanafunzi. Pia unaweza kuwaruhusu wanafunzi wakuulize maswali kuhusu wanaelewa nini kuhusu kile unachoenda kukifundisha.

Uwasilishaji wa kiini cha somo. Unaaweza kuandaa maswali pia unaweza kuandaa makundi ya wanafunzi wachache wachache.

Utumizi/utendaji wa wanafunzi. Hapa mwalimu unaandaa mazoezi, kazi ya mwanafunzi binafsi, mazoezi mengine ambayo watafanya wenyewe, maswali ya papo kwa papo au mazungumzo

Kazi ya nyumbani. Haifai hata kidogo kuwafundisha wanafunzi wageni kumaliza kuwafundisha na kuwaacha bila kuwapa zoezi lolote la kufanya. Zoezi hilo linapaswa kuhusisha jinsi ambavyo mwanafunzi amesoma darasani.

Mfano wa zoezi: Mtafute mtu yeyote kule mitaani muulize maswali haya. Wewe ni nani? Unasoma? Umeoa? Je, uraibu wako ni nini? Na kadhalika. Hii itakusaidia sana kujua wapi palipo na udhaifu ili uwee kuwasaidia wanafunzi kama hajaelewa.

Tathmini. Ni lazima kujitathmini wenyewe kama wameelewa au la.

 

Udhibiti wa darasa

Kipengele hiki kinahusu jinsi ulivyopanga darasa. Je, darasa limepangiliwaje? Je, watu wote wako?

Mbinu za ufundishaji – Mbinu zinazopendekezwa ili uweze kulitawala darasa ni mbinu shirikishi. Usiwe mwongeaje tu wewe mwenyewe. Pia tumia mbinu za kuona.

Uimara wa mwalimu – Lazima kama mwalimu ujiamini katika ufundishaji wako. Usionyeshe kuyumba hata kidogo. Kumbuka mara utakapoyumba hawatakuamini tena hata kama ukifundisha vizuri. Kama wakikuuliza swali ambalo hulijui, jaribu kuwashirikisha. Ikiwa na wao hawajui basi waambie utawapatia jibu siku nyingine.

Unahitaji kuwa safi na uwe mbunifu vilevile.

Mwonekano wa darasa. Lazima darasa liwe linaonekana. Kusiwepo na sauti nyingine inayoingia ndani

Matumizi ya ubao au PowerPoint. Vionekane vizuri.

Sauti ya mwalimu. Je, sauti, yako inasikika vizuri? Hakikisha sauti yako inasikika kwa wanafunzi wote. Uwe na uwezo wa kuimudu lugha vizuri.

Ukubalifu wa mambo ambayo hukufundisha au hukupanga kuyafundisha. Wanafunzi wakitaka kufundishwa kitu fulani ambacho wewe hukujiandaa kuwafundisha – itategemea hali ya darasa – wafundishe.

 

[email protected]