Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Utayarishaji wa mitihani katika ufundishaji wa lugha ya pili

June 26th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

HUU ni mchakato wa upimaji wa maarifa au ujuzi ambao wanafunzi wameupata tangu mwanzo wa kozi hadi mwisho wa kozi.

Kipengele hiki ni cha muhimu sana hivyo lazima kifanyike kwa ustadi na ubunifu mkubwa.

Malengo ya mitihani lazima yalenge kupima mambo manne jinsi tulivyoyaainisha ifuatavyo:

i. Ulenge kupima maarifa na ujuzi aliyopata anayejifunza lugha.

ii. Kupima mbinu mbalimbali alizotumia mwalimu kufundishia kama zimeeleweka au la.

iii. Mitihani imelenga kupima mitaala.

iv. Mitihani inapima uwezo wa kuchochea kujifunza maarifa mapya.

Aina za upimaji

Kuna aina mbili kuu za upimaji zinazohusika katika mchakato wa kuandaa mitihani ya wanafunzi.

Upimaji rasmi. Huu ni upimaji unaofanyika mwishoni mwa kozi na hufanyika mara moja tu. Upimaji huu hupima viwango vyote ambavyo alijifunza mwanafunzi katika kipindi chote cha kozi yake.

Upimaji usio rasmi (Upimaji umbaji). Katika aina hii ya upimaji, mwanafunzi anapimwa wakati somo linaendelea. Kwa mfano, kupitia mazoezi, mitihani na kadhalika. Mara nyingine upimaji huu huitwa upimaji umbaji.

Kanuni za upimaji

Katika upimaji kuna kanuni anuai muhimu zinazopaswa kutiliwa maanani ilikufanikisha mchakato huo. Kanuni hizi ni kama zifuatazo:

Muda wa mtihani. Hakikisha unawapa wanafunzi muda wa kutosha wa kujiandaa.

Muundo wa mtihani. Wadokezee wanafunzi kuhusu muundo wa mtihani ulivyo. Hii itawawezesha kujiandaa vyema.

Upeo wa jaribio. Ni muhimu uhakikishe jaribio lako linajikita na kuangazia masuala au nyanja walizojifunza wanafunzi.

Uhalisia. Ni vyema kutilia maanani kwamba jaribio lako lina uhalisia. Lisiwe lakiyakinifu bali lenye uhalisia ili kuwawezesha wanafunzi kulimudu.

Utendaji. Ni vyema uhakikishe kwamba jaribio lako linachochea ubunifu na utendaji miongoni mwa wanafunzi.

Muundo wa maswali. Ili kufanikisha mchakato wa upimaji, ni vyema kutumia muundo unaoondoa utata katika mtihani huo kwa kuyafanya maswali yawe bayana au yawe wazi.

Muda. Muda wa kufanya mtihani unapaswa kuwa wa kutosha.

Nakala safi. Hakikisha pia kuwepo na umakini katika uandishi. Epuka makosa ya hijai au upigaji chapa.

Jaribio. Hakikisha hurudii majaribio.

Ukweli. Zuia udanganyifu.

 

[email protected]