Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Viambajengo muhimu katika utamaduni wa Kiswahili

September 18th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

Ndoa na Harusi – Hiki ni kipengele kingine muhimu chenye uzito Uswahilini kwa kuwa ni taasisi ya kwanza katika maisha ya kila mtu awe mwanamke au mwanamme.

Ubikira ni ada nyeti inayopatiwa kipaumbele hususan miongoni mwa wanawali wa Kiswahili kabla ya kuolewa. Hii ni kwa sababu ndoa ndicho kitovu cha maisha ya Waswahili. Kwa mintarafu hii, ni desturi ya Uswahilini kwa wazazi kuwa washauri wakuu wa ndoa za watoto wao.

Mama hutakiwa kumshauri bintiye na kumwandaa kwa ndoa kwa kumfunza mambo muhimu mathalan usafi, upishi, kuhifadhi ubikira wake hadi atakapofunga nikahi, jinsi ya kumtunza na kumfurahisha mumewe na kadhalika.

Kwa upande wao, kina baba wana jukumu la kuwafundisha wana wao jinsi ya kuwa wanaume halisi kwa kuwa na sifa kama vile ujasiri, uwezo wa kufanya maamuzi ya busara, kuwajibika, kumtunza mkewe na familia yake na mengineyo.

Ni muhimu kuelewa kuwa kuna hatua kadha muhimu zinazohusika tangu mwanamme anapopeleka posa kwa mwanamwali anayetaka kumwoa hadi anapotoa mahari na hatimaye kulishana yamini ya kuishi pamoja kama mume na mke katika ndoa.

Kando na wazazi, kipindi hicho huwashiriki makungwi na masomo katika kuwaelekeza na kuwafundisha maharusi kabla na baada ya sherehe ya harusi. Kwa kawaida kwa Waswahili ambao wengi wao ni Waislamu, sharia za Kiislamu huwa ndicho kigezo pekee cha kuendeshea maisha ya ndoa.

Mazishi – Hii ni daraja muhimu inayoashiria mpito wa maisha ambapo waja hurejea walikotoka na muhimu zaidi kuwakumbusha walio hai juu ya marejeo hayo kwa Mola wao. Kwa Waislamu wote wa ujiranini, msiba wa kufiliwa huwa ni faradhi-kifaya. Huzuni za kufiliwa huwa ni za wote na kazi kubwa ya majirani na marafiki ni kuwafariji wenzao waliopatwa na msiba.

Kwa kawaida katika, msiba unapozuka, kazi zote, kuanzia utoaji wa habari za kifo, uchimbaji ufuo, uoshaji, uchimbaji kaburi, kupatikana kwa tusi, uchukuaji wa jeneza, uzikaji na sala zote za kumsalia maiti huwa ni za jumuiya.

Wanajamii wote ni sharti wahusike kwa namna moja au nyingine. Kimsingi, muda wa maombolezi huchukua siku arubaini ambapo baada ya hapo, ada ndogondogo kama vile kupiga dua na kufagillia mavani mara kwa mara na kila mwaka daima huzingatiwa.

[email protected]

Marejeo

Nurse D. na Spear Th. (1985.) The Swahili: Reconstructing the History and Language of an African Society, 800-1500. Philadelphia.

Sengo T.S.Y. (1985). The Indian Ocean Complex and the Kiswahili folklore:The case of Zanzibarian Tale-Performance. Unpublished Ph.D                thesis. Khartoum University.

Shariff I.N. (1988). Tungo Zetu. Trenton: The Red Sea Press, Inc.