Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vigezo muhimu katika ufunzaji wa ama Riwaya au Tamthilia

August 7th, 2019 3 min read

Na WANDERI KAMAU

UFUNDISHAJI wa riwaya na tamthilia au fasihi yoyote unahitaji mwongozo wa nadharia fulani ya uhakiki.

Kimsingi, riwaya na tamthilia hutegemea nyenzo kuu maalumu ili zijengeke.

Ni kazi ya mwalimu kutumia mifano mbalimbali ili kuwafahamisha wanafunzi nyenzo hizo.

Mwalimu anapaswa kushughulikia dhamira na maudhui, wahusika, mtiririko wa matukio, mazingira au mandhari, muundo na mtindo.

Katika kufundisha kipengele cha mazingira au mandhari, mwalimu atilie maanani kwamba misingi ya fasihi imejikita katika jamii.

Mwandishi ni mtu aliyezaliwa na jamii fulani, katika mazingira fulani na wakati fulani. Yale yote anayozungumzia yanatokana na tajiriba yake katika jamii.

Mwalimu wa fasihi awaelekeze wanafunzi katika muktadha wa kijamii na kihistoria ambao mwandishi anazingatia katika kazi zake.

Kwa mfano, ili wanafunzi waielewe vizuri tamthilia ‘Mashetani’ yake Ebrahim Hussein, itabidi mwalimu afunze kwa kurejelea historia ya Tanganyika na Unguja kabla na baada ya mapinduzi ya Januari 1964 na Azimio la Arusha la 1967.

Ikiwa ni wahusika, mwalimu azingatie vile wanavyojitokeza katika hadithi. Awasaidie wanafunzi kutambua wasifu wa nje na wa ndani wa wahusika hao.

Wana sura au maumbile gani? Wana tabia gani? Wametumiwaje? Wana dhamana zipi? Tabia/wasifu wao utaonekana kwa kuzingatia vitendo vyao, lugha yao, mavazi yao, uhusiano wao na wahusika wengine, na maelezo yanayotolewa na wahusika wengine au mwandishi kuwahusu.

Wanafunzi waelekezwe kuwatambua wahusika wakuu, wadogo, bapa, mviringo, foili, shinda na wengineo. Mwalimu awape wanafunzi nafasi ya kujadiliana masuala nyeti yanayowahusu wahusika.

Mwalimu ajadiliane na wanafunzi kuhusu mtiririko wa matukio katika vitabu wanavyosoma. Baadhi ya maswali yafuatayo yanaweza kuzingatiwa: Kisa kinahusu kina nani? Ni matukio yapi yanayorejelewa? Ni nani anayeelekea kutawala matukio? Matukio haya yanatokea wapi? Matukio haya yanasababishwa na nini? Matukio hayo yana uhusiano upi na yaliyotangulia/yanayofuata?

Kwa mujibu wa mafunzo haya, mwalimu aingize wazo la upeo au kilele. Mwalimu pia awaelekeze wanafunzi kuitambua lugha ilivyotumiwa kujenga mtiririko wa matukio, kisa na hata kuibusha hisia na maudhui mbalimbali.

Hatimaye, kwa kuzingatia vipengele vyote vilivyopitiwa, mwalimu awasaidie wanafunzi wake kutambua maudhui ya kazi husika kwa kuzingatia vipengele vyote vinavyojenga riwaya au tamthilia. Mwalimu atawasaidia wanafunzi kuyatambua maudhui kwa kuwapa maswali yanayowaelekeza, kama: Ni maudhui yapi yanayojitokeza katika kazi hii? Maudhui ya kazi hii yanakuzwaje na wahusika? Maudhui ya kazi hii yanaendelezwaje na lugha na mtindo uliotumiwa? Ni migogoro gani inayojitokeza katika kazi hii? Je, migogoro hii imesuluhishwa? Tunapata funzo gani katika kazi katika hii? Fasihi inatakiwa ifundishwe kwa mtindo utakaowapa wanafunzi nafasi ya kuhisi ukweli na uhalisia wa matukio mbalimbali yasimuliwayo.

Stadi za lugha 

Stadi zote za lugha (kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika) zihusishwe.

Wanafunzi wasikilize maelezo ya mwalimu, vipindi vya redio au kanda kisha wajadiliane kuhusu waliyoyasikia. Wasome vitabu na majarida mbalimbali, na mwisho waandike na hata kuigiza waliyoyasoma.

Kwa kuzingatia haya, baadhi ya matatizo ambayo yamekuwa yakijitokeza katika ufundishaji wa fasihi huenda hatimaye yakaepukika.

Ni dhahiri kwamba utegemezi wa miongozo chapwa limekuwa tatizo kuu ambalo limekuwepo kwa muda mrefu katika ufundishaji wa fasihi katika taasisi nyingi za elimu, hasa shule za upili, taasisi za walimu na vyuo vikuu.

Matokeo ya ufundishaji huo duni yamekuwa ni uwepo wa wanafunzi wasiofahamu undani wa masuala muhimu ya fasihi, hivyo kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa.

Pili, wanafunzi wengi hupoteza hamasa ya kusoma vitabu vingi vya kubuni, mbali na vitabu tahiniwa vya fasihi.

Wengi huviona vitabu hivyo kama “mzigo” kutokana na kutopewa hamasa na walimu wao, hasa katika utafiti kuhusu mbinu muhimu, mathalani ujenzi wa maudhui, wahusika, matumizi ya mbinu za lugha kati ya nyenzo nyingine kuu muhimu za fasihi.

Hata hivyo, hili linaweza kubadilika ikiwa wanafunzi wenyewe pia watajenga ari ya kuvichangamkia vitabu vya fasihi ili kupanua ufahamu wao wa lugha. Hili bila shaka litaibua msisimko wa aina yake na mapambazuko mapya katika ufunzaji na uandishi wa fasihi.

 

[email protected]