Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vipengele vikuu vinavyotofautisha Isimu na Isimujamii

February 20th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

KULINGANA na Mgullu akimrejea Hartman (1972), Isimu ni eneo maalum la mtalaa ambalo lengo lake huwa ni kuchunguza lugha.

Wanaisimu huzungumza lugha zikiwa ni nyenzo muhimu za mawasiliano ya mwanadamu.

Mtazamo huu wa wanaisimu Massamba, Richard na wenzake pamoja na Hartman unaafiki kwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kwamba katika fasili zao jambo la msingi linalosisitizwa ni kwamba, Isimu hushughulikia uchunguzi wa lugha mbalimbali kwa kutumia misingi ya kisayansi.

Ni kutokana na shughuli ya kuchunguza isimu ndiposa isimu inafafanuliwa kama sayansi ya lugha.

Pamoja na hayo vilevile kwa upande mwingine fasili hizi zimeweka msisitizo katika mfumo wa mawasiliano ya wanadamu.

Kwa mujibu wa fasili hizi bila shaka tunaweza kusema isimu na mwanadamu ni vitu ambavyo hushikamana kama pande mbili za sarafu ambazo si rahisi kuzitenganisha.

Aidha, fasili za wataalamu hawa zinadhihirisha bayana kwamba, isimu na isimujamii ni sawa na pande mbili za sarufi moja ambazo hutofautiana maadamu zina picha mbili tofauti zisizoweza kutenganishwa bila kupoteza thamani ya sarafu.

Tofauti na mkamilishano kati ya isimu na isimu jamii zinaweza kufafanuliwa kupitia vipengele vifuatavyo: ukongwe,  uchangamani, na maana.

Ukongwe

Tofauti mojawapo kati ya isimu na isimujamii inajitokeza katika kipengele cha umri. Isimu ni taaluma kongwe sana ukilinganisha na isimu jamii.

Kulingana na Mekacha  akiwanukuu Viktoria Fromkin na Robert Rodman, ni kuwa isimu ilianza huko Uarabuni mwaka 1600 kabla ya Kristo.

Kwa upande mwingine,  isimujamii ilianza miaka ya 1950 na 1960, na kupata mashiko zaidi kwenye miaka ya 1960 na 1971 ambapo machapisho mengi ya isimujamii yalianza kuonekana.

Pia ni taaluma ambayo ilizaliwa kutokana na taaluma nyingine za isimu na zisizo za isimu.

Uchangamani

Katika kipengele hiki tunaona kwamba isimujamii ni taaluma yenye uchangamani kwa maana kuwa inahusisha taaluma mbili ambazo ni isimu na jamii ilhali isimu yenyewe si taaluma changamani.

Maana

Isimu na isimujamii hutofautiana katika maana. Jinsi tulivyotaja awali, isimu yenyewe ni taalauma inayozingatia ufafanuzi, uchambuzi na uchunguzi wa lugha kwa kutumia mbinu za kisayansi, wakati isimujamii ikiwa ni taaluma inayoshughulika na uchunguzi unaolenga kufafanua uhusiano uliopo kati ya lugha na jamii.

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo:

   Msanjila, Y. P. (1990) “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili ni Teacher Training Colleges in Tanzania”.                  Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318

   Mtembezi, I. J. (1997). Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia”. Dar es Salaam: BAKITA.

   Mulokozi, M. M. (1991) “English versus Kiswahili ni Tanzania’s Secondary Education”. Swahili Studies Ghent.