Habari za Kitaifa

Ukuruba wa Ruto, Raila unaelekea 2027, wanasiasa wafunguka


CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Rais William Ruto na kile cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Raila Odinga vimeonyesha dalili za kushirikiana au kuungana kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Viongozi wa vyama hivyo Jumamosi walisema kuteuliwa kwa viongozi wa ODM katika baraza la mawaziri la serikali ya Kenya Kwanza ni kiashirio cha kwanza kuwa ushirikiano kama huo unanukia.

Walisema hayo wakati wa sherehe ya kutoa shukrani kufuatia uteuzi wa Waziri wa Ustawi wa Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogo Wycliffe Oparanya, iliyohudhuriwa na Rais William Ruto eneo la Butere, Kaunti ya Kakamega.

Rais Ruto ndiye aliyetoa dokezo la kwanza aliposema kuwa serikali jumuishi iliyoundwa na Kenya Kwanza na ODM haikuwa ya muda tu.

Alisema baadhi ya ahadi zilizoko kwenye  manifesto za Kenya Kwanza na ODM zinafanana na hivyo haitakuwa vigumu kwa mirengo hiyo miwili kushirikiana.

“Baadhi ya ahadi zinazofanana katika manifesto za Kenya Kwanza na ile ya ODM ni pamoja na Mpango wa Afya kwa Wote, Mpango wa Ujenzi wa Nyumba za Gharama Nafuu, Ustawi wa Biashara Ndogo Ndogo, Ustawi wa Kiviwanda katika Maeneo ya Mashambani, miongoni mwa nyingine,” akasema Rais Ruto.

Alisema kuwa falsafa za UDA na ODM zinafanana ikizingatiwa kuwa amewahi kuhudumu kama naibu kiongozi wa ODM na hivyo anaelewa mengi kuhusu chama hicho cha chungwa.

“Namshukuru ndugu yangu Raila Odinga kwa kukubali kufanya kazi nami. Tunataka kushirikiana kikazi huku tukiweka mbele maslahi ya nchi. Wakati huja ambapo maendeleo, ustawi na umoja wa kitaifa hupewa kipaumbele kuliko chochote kile,” Rais Ruto akasema.

Viongozi ODM ambao Rais aliwateua kuwa mawaziri katika serikali yake ni waliokuwa manaibu wa kiongozi wa chama Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika) na Hassan Ali Joho (Madini), aliyekuwa Mwenyekiti wa ODM John Mbadi (Fedha), aliyekuwa Katibu wa Masuala ya Kisiasa katika chama hicho James Opiyo Wandayi (Kawi) na mwanachama wa Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Chaguzi katika ODM Beatrice Askul Moe (Masuala ya Afrika Mashariki)

Maafisa hao walijiuzulu nyadhifa zao baada kabla ya kupigwa msasa na kamati ya bunge la kitaifa kuhusu uteuzi kubaini ufaafu wao kwa nyadhifa hizo.

Kwa upande wake Naibu kiongozi wa ODM Simba Arati alisema kuanzia sasa  watafanya kazi na Rais Ruto kwa lengo la kuleta utulivu nchini Kenya.

Bw Arati ambaye ni Gavana wa Kisii, aliwataka viongozi wanne wa ODM walioteuliwa kuhudumu katika baraza la mawaziri wa Rais Ruto kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili “kufikia uchaguzi mkuu ujao tutakuwa na timu yenye nguvu.”

“Kuanzia sasa tunataka kutembelea pamoja kama Wakenya ili tujenge taifa letu. Ingawa hatuna makubaliano na Kenya Kwanza, tulipeana viongozi wetu wakuu kumsaidia Rais Ruto na tutaona ikiwa tutatembea pamoja 2027. Tunataka kushirikiana na kudumisha umoja kuendelea mbele,” akasema Bw Arati.

Gavana huyo wa Kisii alisema maeneo ya Magharibi na Nyanza yanaendeleza mikakati ya kutwaa urais baada ya Rais Ruto kukamilisha mihula yake miwili uongozini.

“Eneo la kati limeonya urais na ni sisi pia tupate nafasi. Jamii za Wakisii, Waluo na Waluhya zitasimama kidete Ruto atakapokamilisha uongozi wake,” akaongeza.

Gavana wa Siaya James Orengo alisema mnamo 2007 taifa lilikumbwa na ghasia za baada ya uchaguzi, Wakenya waliungana na kuunda serikali ya muungano na utulivu ukarejea nchini.

“Nina uhakika kwamba kwa chini ya ushirikiano wa sasa, Kenya inaweza kurejelea hali nzuri,” anasema Bw Orengo.

Gavana huyo wa Siaya alimshukuru Rais Ruto kwa kuteua viongozi wa ODM katika serikali yake bila kulazimisha chama hicho kuvunjwa na kujiunga na serikali.

Miito mingine ya kuhimiza ushirikiano kati ya UDA na ODM ilitolewa na Gavana wa Busia Paul Otuoma ambaye pia alimhongera rais kwa kushirikisha wanachama wa ODM katika baraza lake la mawaziri.

“Kuanzia sasa, ikiwa mambo yatakuwa mazuri, tutaungana na Rais Ruto,” akasema Bw Otuoma.

Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi alisema wakazi wa Nyanza wakisema ndio, huwa hawabadilishi msimamo.

“Rais amefungua ukurasa mpya wa uongozi nchini. Amewateua viongozi wa upinzani katika serikali yake na hilo ni jambo la kupewa uzito. Nakushukuru kwa kuanza safari ya kuleta Wakenya pamoja,” akasema.

Bw Oparanya alifichua urafiki wa muda mrefu kati yake na Rais akisema ni mojawapo ya sababu za kuteuliwa kwake kuhudumu katika serikali ya Kenya Kwanza.
“Tumekuwa tukiongea lakini nyakati zingine mawimbi ya mawasiliano hufeli. Hatimaye mawimbi hayo ya mawasiliano ni shwari na sasa ninaahidi kukuhudumia kwa uaminifu,” Bw Oparanya akasema.