Habari za Kaunti

Ukusanyaji wa mapato Nairobi wasalia ‘pasua kichwa’

January 25th, 2024 1 min read

NA WINNIE ONYANDO

SUALA la kutambua kwa kina namna wavuti maalum wa kukusanya mapato Kaunti ya Nairobi inavyofanya kazi, linaendelea kuwa pasua kichwa.

Kamati maalum iliyoundwa kuchunguza mfumo wa ukusanyaji mapato jijini Nairobi, ambao unajulikana kama Nairobi Revenue Services (NRS) inaendelea kuwa na maswali mengi kuliko majibu.

Akizungumza Jumanne baada ya kukutana na maafisa kutoka Shirika la Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA), mwenyekiti wa kamati maalum ya kuchunguza masuala ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato Nairobi, Peter Imwatok, alisema kwamba watafuatilia suala hilo hadi mwisho.

“Kwa sasa, haijulikani ni nani anatawala au kuongoza mfumo huo. Hii ndiyo maana tunataka maafisa husika kufika mbele ya kamati ili ibainike ni mfumo gani haswa unaotumika kukusanya mapato,” akasema Bw Imwatok.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya watu wawili wanaofanya kazi katika afisi za St Peter Cleavers Revenue eneo la Starehe kukamatwa kwa kujihusisha na ulaghai.

Mwaka 2023, kamati hiyo ilielezea wasiwasi wake kuhusu mchakato wa ukusanyaji na usimamizi wa mapato.

Hii ilimfanya Gavana Johnson Sakaja kujitetea akisema kwamba serikali yake inatumia wavuti maalum kukusanya mapato, inayojulikana kama Nairobi Revenue Services (NRS).

Kwa sasa, kamati hiyo inaendelea kufuatilia masuala yote ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato.