Makala

UKUZAJI MBOGA: Mama anayefanya makuu kwa kukuza mboga za aina mbalimbali

September 5th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KAZI ya ukulima imempa Bi Mary Gichui ajira tosha inayomwezesha sasa kujisimamia na kukimu mengi ya mahitaji yake na ya familia aliyo nayo katika eneo la Gitaru, kaunti ndogo ya Kikuyu.

‘Mama Githinji’ kama anavyojulikana sana miongoni mwa wanakiji wenzake, alijitosa katika kilimo cha mboga za sampuli mbalimbali yapata miaka 20 iliyopita.

Baada ya kudadisi hali yake maishani, aliona kwamba lazima afanye jambo ambalo litamwezesha kupata riziki ya kila siku.

Wazo lililomjia haraka haraka ni la kujishughulisha na kilimo ili ajiajiri badala ya kutafuta kazi ya kuajiriwa.

Alipoanza shughuli za ukulima, alianza katika sehemu ndogo tu ya shamba lake huku akikuza kabeji.

Baadaye alipanua sehemu ya ardhi yake kwa minajili ya kilimo.

Kufikia sasa ana shamba la takriban ekari tano ambako anakuzia aina tofauti za mboga kama vile kabichi, sukumawiki, mchicha, mwangani, mnavu, terere, na mboga nyinginezo za kiasili.

Katika shughuli za kila siku, Bi Gichui hufika shambani tayari kwa kazi ya kushughulikia mimea yake na kuitunza.

Kwa kawaida, ana wafanyakazi kati ya 13-15 ambako watano hunyunyizia mboga zote shambani maji na wengine wanane ama kumi huhusika katika kupalilia. Aidha, kazi ya Bi Gichui hufuatilia shughuli zote zinazofanyika shambani kuhakikisha ya kuwa mboga zote zimenyunyiziwa maji na pia zimepaliliwa.

Zaidi huwa anahusika katika kuuza mazao yote pale shambani ambapo wateja wake huingia shambani na kuchuna aina wanazotaka za mboga, na kisha kumletea kwake kupimiwa viwango na kuuziwa.

Bi Gichui, hununua mbegu zake katika shirika la East African Seed, ambazo zimeidhinishwa na Wizara ya Kilimo. Kwa kawaida, huziandaa mbegu zake za mboga katika sehemu moja ya shamba kwa muda wa hadi mwezi mmoja, kabla ya kuzihamisha na kuzipanda katika sehemu nyinginezo shambani.

Muda wa mwezi mmoja

Baada ya uhamisho huu, huwa zinachukua muda wa mwezi mmoja na kuwa tayari kwa mavuno.

Katika muda huu shughuli za kupalilia huwa zinaendeshwa na kunyunyiziwa maji kila siku.

Baadhi ya mimea mingine kama vile mboga za sagaa, cancilla, terere na saget huchukua muda mfupi wa mwezi moja na nusu kukomaa na kuwa tayari kwa mavuno.

 

Bi Mary Gichui (kulia) awauzia baadhi ya wateja wake mboga katika eneo la Gitaru, Kikuyu, Kaunti ya Kiambu. Picha/ Chris Adungo

Kwa kawaida, mboga nyingi huvunwa kila baada ya siku 10 ambapo mavuno yanaweza kufanyika katika muda wa miezi sita na zaidi hasa kwa sukumawiki na mchicha.

“Kilimo hiki huwa nakifanya kwa kutumia mbolea ya kiasili kutoka kwa kuku na wakati mwingine nanunua ile mbolea ya madukani kwa lengo la kuboresha kukua kwa mimea hii yote,” anaeleza Bi Gichui.

Pia kuna baadhi ya mimea ambayo huhitaji kunyunyiziwa dawa ya kupigana na wadudu, na katika muda wa siku 14, sehemu ambayo dawa hii imetumika hamna mavuno ambayo hufanyika. Shamba hili lake huwa linanyunyiziwa maji na mashine inayotoa maji katika kijito kinachopita shambani mwake na kuyaeneza maji kutumia mifereji.

Kulingana naye, wateja kati ya 20- 30, wengi wao wakiwa wafanyibiashara wadogo wadogo hufika shambani mwake kutoka maeneo ya Kikuyu mjini, Gitaru na Dagoretti.

Kwa kawaida, huwa wanafika humu shambani kila siku kwanzia Jumatatu hadi Jumamosi ili kupata bidhaa muhimu wanazohitaji. Anauzia wateja wake kulingana na kiasi wanachohitaji.

Zaidi huwa anauza kabichi katika shule 12 za upili katika kaunti hii ya kiambu, kati ya kilo 300 na 1,000 kulingana na mahitaji ya shule husika.

Mauzo haya huwa anayafanya kila siku ya Jumatatu na Alhamisi na kuuza kwa bei ya kati ya shilingi ishirini na hamsini kwa kilo moja kulingana na msimu.

Kilimo hiki, kulingana naye kina manufaa makubwa kwake kwani kinampa riziki ya kila siku na pia kimemwezesha kupata mapato ya kuwaelimisha wanawe wanne ambao baadhi yao wamesoma hadi vyuo vikuu.