Makala

Ukuzaji wa mboga mseto za kienyeji Nairobi unampa mapato ya kuridhisha

May 21st, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KILIMO cha mboga ndicho ofisi ya Florah Wambui na tunampata akichumia mmoja wa wateja wake, akiwa mwingi wa bashasha.

Mama huyu ambaye ni mkwasi wa tabasamu, hukuza mseto wa mboga asili za kienyeji eneo la Mwiki, kaunti ya Nairobi.

Shamba lake la kukodi na lenye ukubwa wa karibu nusu ekari, limesitiri mboga aina ya managu maarufu kama sucha, saga na kunde.

Kabla ya kuvalia njuga masuala ya kilimo, Wambui, 44, alikuwa mfanyakazi wa kawaida katika shirika la reli nchini kwa muda wa miaka mitatu.

“Pamoja na wafanyakazi wenza, tulikuwa tuking’oa nyasi zinazomea kwenye barabara ya garimoshi,” aeleza Bi Wambui.

Anadokeza kwamba alikuwa akihudumu kati ya mtaa wa Kahawa West hadi Dandora, Nairobi.

Ni kupitia kazi hiyo ambapo mama huyu alivutiwa na wakulima waliopanda mimea kandokando mwa reli. Alishawishika na kujiunga na wakulima hao, akapata kipande kidogo cha ardhi kandokando mwa reli akakuza mboga.

“Ilinigharimu Sh200 pekee, ambapo nilinunua mbegu za kunde. Wiki tatu baadaye, nilipofanya mauzo nilipata faida ya Sh600,” aelezea mkulima huyu.

Anaongeza kusema kuwa shughuli za kulima, palizi na kuvuna, yeye ndiye alijifanyia.

Mwaka wa 2017, Wambui ambaye ni mama wa watoto wanne anasema aliacha kazi katika shirika la reli ili kufanya kilimo kikamilifu.

Machi mwaka uliopita, 2018, alipata kipande cha shamba anacholima kwa sasa eneo la Mwiki, na ambacho ni cha kukodi.

“Kukodi mashamba eneo hili ni kwa kipekee, kwani huwa na mkataba wa makubaliano na kutoa ada mara moja. Nililipa Sh20,000 kwa mujibu wa muda ambao nitafanya kilimo,” afafanua.

Soko la mboga asili za kienyeji kama vile mchicha, managu, kunde, kansella, saga na mito, ni mithili ya mahamri moto mjini.

Aliamua kukuza kunde, saga na managu kwa sababu zinachukua muda mfupi kuwa tayari kwa mavuno.

“Baada ya wiki tatu, huanza kuvuna kunde, managu na saga huvuna wiki ya nne na tano baada ya upanzi,” asema mwanazaraa huyu.

Ili kukabiliana na kizingiti cha upungufu wa shamba, Bi Wambui huchanganya mbegu za aina hizo tatu za mboga na kuzipanda.

Kilo moja ya kunde hugharimu kati ya Sh50-100, kulingana na msimu. Mkulima huyu anasema managu huwa bei ghali, kilo mbili zikigharimu Sh1,500. Mbegu za saga kilo mbili huuzwa Sh1,200.

“Saga unapokuza mara ya kwanza, huhitaji kununua mbegu tena kwani huziachilia kukomaa ili kupata mbegu,” anasema.

Bi Florah Wambui, mkulima wa mboga katika kaunti ya Nairobi. Picha/ Sammy Waweru

Hulima karibu majembe mawili kuenda chini, kisha anaruhusu makwekwe kukauka pamoja na udongo kutulia, kwa siku kadhaa. Wataalamu wa masuala ya kilimo wanasema kwa kufanya hivyo, wadudu walioko hufariki kwa kukosa lishe.

“Makwekwe huchangia usambaaji wa wadudu na magonjwa, yanapokauka husaidia kudhibiti changamoto hizo,” anasema Caroline Njeri, mtaalamu kutoka Safari Seeds. Kulingana na mdau, anapendekeza kupewa muda wa karibu wiki mbili.

Bi Wambui anasema huchanganya udongo na mbolea, anayouziwa Sh200 gunia la kilo 90 akijumuisha gharama ya usafirishaji moja linakuwa jumla ya Sh250.

“Upanzi ninaofanya hauhitaji taratibu za mashimo wala mitaro, humwaga tambarare mchanganyiko wa mbegu za mboga ninazokuza halafu ninapampu maji,” aelezea. Ana jenereta ya shughuli hiyo aliyoinunua Sh23, 000 kupitia mazao ya kilimo.

Pembezoni mwa shamba lake, amepakana na mto unaosemekana kuwa mpaka wa kaunti ya Nairobi na Kiambu. Hutumia maji hayo kufanya kilimo.

Kilo moja ya mboga anazopanda, haipungui Sh30. Wateja wake ni wa kijumla, na ambao huziendea shambani mwake.

Wakati wa mahojiano, Wambui aliambia Taifa Leo Digitali kwamba akiondoa gharama ya matumizi, kila mwezi hakosi kutia kibindoni zaidi ya Sh20, 000.