Makala

Ukuzaji wa miche ya matunda, miti na maua waendelea kuajiri vijana

May 17th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KANDOKANDO mwa barabara nyingi nchini hutakosa kuona biashara tofauti zikiendeshwa.

Kuanzia uoshaji wa magari, mikahawa, sanaa za uchoraji na uchongaji vinyago, uuzaji wa bidhaa mbalimbali, ni baadhi tu ya biashara utakazoona.

Ukuzaji wa miche ya matunda na miti ya kurembesha mazingira na ya kuyaimarisha pamoja na maua, pembezoni mwa barabara ni biashara inayoendelea kunoga.

Nafasi za ajira Kenya ni haba mno, na kadri miaka inavyozidi kusonga ndivyo vijana wengi wanaendelea kufuzu kwa vyeti mbalimbali vya masomo kutoka taasisi za juu za elimu.

Ni kutokana na changamoto za aina hiyo, ambapo wengi wanatafuta njia mbadala kuzimbua riziki, vyeti vya masomo waliyopata wakilazimika kuviweka sandukuni. Kilimo ni mojawapo ya sekta ambazo wengi wao wamekimbilia kusukuma gurudumu la maisha.

Katika viunga vya miche inayokuziwa kandokando mwa barabara, hutakosa kuona vijana wakiishughulikia. Aidha, kuna wanaomiliki na wengine kuajiriwa.

Ajira kwa vijana

Eneo la Kabati, Murang’a pembezoni mwa barabara inayounganisha mji wa Thika na Kenol, Bw James Macharia ana kiunga kilichosheheni miche tofauti tofauti.

Kiunga hicho chenye ukubwa wa ekari moja na nusu, kimesitiri miche ya matunda kama matufaha, maparachichi, stroberi, mapapai, maembe na zabibu.

Pia, kina miche ya maua na mimea ya kusawazisha hewa maskani. “Miche ya matunda na miti ni mingi. Ipo ya macadamia kwa kuwa yanaendelea kuimarisha wakulima wake,” anaeleza Bw Macharia, ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kilimo.

Ni katika kiunga hichohicho, ambapo mwanamazingira huyo amebuni nafasi kadhaa za ajira kwa vijana. “Nina wafanyakazi watatu niliowaajiri kunisaidia. Wakati kazi ni nyingi hutafuta wa muda,” anasema.

Alianza shughuli hii mwaka wa 2008, na kufikia sasa hajutii kamwe kwa ajili ya matunda anayoshuhudia kila uchao. “Kiunga nilichoanza safari nacho kilikuwa chenye ukubwa chini ya thumni ekari (1/8) na ilinigharimu mtaji wa Sh23, 000 pekee,” afichua Bw Macharia, akisisitiza kwamba si lazima mkulima chipukizi na mwenye ari ya kufanya kilimo cha miche awe na kipande kikubwa cha ardhi.

Kilikuwa eneo la Kahawa Sukari, Thika Super Highway.

Anasimulia kuwa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ulipoanza, alilazimika kuhamia Ruiru, Kiambu mwaka wa 2009.

Mnamo 2010, Macharia alipata kiunga kikubwa alichoko kwa sasa Kabati, Murang’a.

Muhimu kuzingatia

Ili kufanikisha ukuzaji wa miche, mkulima anahimizwa kulenga sehemu yenye chanzo cha maji safi na ya kutosha. Mtaalamu huyu anasema miche, ambayo ni mimea michanga, inahitaji maji mengi ili kuinawirisha. “Kilichonifanya nihamie hapa ni kuwepo kwa maji ya kutosha, na ni eneo la chemichemi,” asema.

Kauli ya mdau huyu wa kilimo kuhusu maji, inatiliwa mkazo na Bw Richard Maina, ambaye pia ni mkuzaji wa miche kaunti ya Nyeri. “Kilimo chochote kile kinategemea maji. Miche hubembelezwa kwa maji ili istawi,” anasema Bw Maina.

Mkulima huyu ambaye pia amebuni nafasi kadhaa za ajira kwa vijana amewekeza pakubwa katika kilimo cha miche pembezoni mwa Mto Chania, ulioko mita chache kutoka mji wa Nyeri.

Maji ya Mto Chania hutoka Mlima Aberdares.

Bw Maina hukuza miche ya miti na matunda. Hali kadhalika, ana miche ya maua aina mbalimbali.

“Ninahimiza wakulima tupande miti kwa wingi ili tuweze kuhifadhi mazingira na vyanzo vya mito yetu,” anahimiza Bw Maina, akiongeza kwamba ukuzaji wa miche una uwezo kuajiri vijana wengi nchini.

Wanamazingira hawa kwa kauli moja wanaafikiana kwamba katika kilimo chochote kile, haja ipo mkulima kujua kiwango cha asidi (pH) ya udongo wa shamba lake. Kwa kawaida mimea hustawi kwenye udongo wa pH kati ya 6.0-7.5.

Msimu wa mvua, biashara hii hunoga kwani wengi hutumia fursa ya maji ya mvua kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti na matunda.

Miche wanayopanda wanazaraa hawa hugharimu kati ya Sh10 hadi Sh500.

Ili kuimarisha soko, unashauriwa kufanya matangazo kupitia mitandao kama vile Facebook, Tovuti, Twitter, Instagram na hata Whats App. Vyombo vya habari pia ni njia nyingine ya kufanya mauzo ya bidhaa.