Habari

Ukuzaji wa mipamba kwa ajili ya kupata pamba kuinua viwanda vya nguo nchini

November 26th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

UKUZAJI wa mipamba kwa ajili ya uzalishaji wa pamba unavipa viwanda vya nguo nguvu na uhai wa kujiendeleza.

Hivi majuzi kampuni ujumbe wa Thika Cloth Mills, ilizuru eneo la Nyanza kwa lengo la kutafuta soko la pamba ili kununua kutoka kwa wakulima.

Ujumbe wa watu wanane kutoka kampuni hiyo ulizuru kaunti za Homa Bay, Kisumu, na Siaya kwa lengo la kutafuta soko la kununua pamba kwa wingi.

Kwa wakati huu kampuni mbili za kuunda nguo za majora; Thika Cloth Mills na SunFlag Textile pamoja na Knit Wear Manufacturing Ltd zimejitolea mhanga kuona ya kwamba zinanunua pamba kutoka kaunti kadha za eneo la Nyanza.

Mkurugenzi wa Thika Cloth Mills Bi Tejal Dhodhia alithibitisha kuwa serikali imejitolea kuona ya kwamba wakulima wanapewa mbegu za pamba na dawa za kupuliza kwa zao hilo la pamba.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Thika Cloth Mills Bi Tejal Dhodhia (kulia) akihutubia viongozi wa Kaunti ya Homa Bay walipozuru eneo hilo Novemba 2019. Picha/ Lawrence Ongaro

Wakati huo pia kampuni hiyo ya kushona majora ya nguo imepewa zabuni na serikali kushona nguo za idara ya usalama.

“Lengo letu kuu katika mikakati hiyo ni kuona ya kwamba ‘tunahubiri’ ajenda nne muhimu za serikali katika kaunti zote 47,” alisema Bi Dhodhia.

Meneja mkuu wa kampuni ya SunFlag Textile na Knitwear Manufacturing Ltd, Bw Vassan Shah, alisema kampuni hiyo inanunua pamba kwa wingi kutoka Uganda lakini watalenga kuzuru maeneo tofauti kukutana na wakulima wa pamba hapa nchini ili wanunue bidhaa hiyo kutoka kwao.

“Tungetaka kuona wakulima wa pamba wakinufaika pakubwa baada ya sisi kununua pamba kutoka kwao,” alisema Bw Shah.

Kaunti ya Homa Bay ilikaribisha ujumbe huo kutoka Thika huku madiwani (MCA) wakisema watawahamasisha wakulima ili wajihusishe na kilimo cha pamba.

Diwani wa eneo hilo Bw Julius Nyambu ambaye ndiye mwenyekiti wa idara ya kilimo, alisema ahadi ya kampuni hizo kutoa hakikisho la kununua pamba kwa Sh52 kwa kilo moja ni hatua kubwa ya kupongezwa.

“Mpango huo umekuja wakati mzuri kwa sababu hapo awali wakulima wa pamba walilipwa pesa duni kabisa baada ya kupoteza matumaini,” alisema Bw Nyambu.

Afisa mwingine wa kamati ya kilimo Bw Anguko Juma aliwapeleka wageni hao wa Thika kwenye shamba lake la pamba.

Alisema mswada utapitishwa bungeni ili kushinikiza wakulima wenye mashamba yaliyo wazi wayatoe kwa serikali ili mipamba ipandwe mle ndani.

Bw Anguko alisema kwa sasa kuna wakulima wapatao 1,600 lakini wanalenga wapige hatua wafike 10,000 kwa siku za hivi karibuni.

Ziara Siaya

Ujumbe huo wa kutoka Thika Cloth Mills pia ulizuru pia Kaunti ya Siaya ambapo walikaribishwa vyema na viongozi wa sehemu hiyo.

Kulingana na Bi Dhodhia, wakazi wa Siaya wamejitolea kustawisha pamba kwa wingi ili nao waweze kujiinua kiuchumi wakiuzia kiwanda hicho zao hilo muhimu.

“Tayari tumezungumza na viongozi wa hapa na wametuhakikishia ya kwamba wakazi wa hapa wamejitolea kurejelea kilimo cha zao hilo ambalo lilikuwa na thamani kubwa miaka ya themanini,” alisema Bi Dhodhia.

Alisema iwapo pamba itavunwa kwa wingi, bila shaka kampuni za kushona nguo zitarejelea sifa zao za hapo awali za kushona majora na kuinua uchumi wa nchi kwa kiwango kikubwa.