Makala

Ukuzaji wa miparachichi unamkimu kimaisha

August 21st, 2020 3 min read

Na SAMMY WAWERU

Miaka miwili baada ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Masuala ya Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), Boniface Mathenge alianza kutekeleza kwa njia ya matendo aliyosoma darasani.

Kijana Boniface ni mhitimu wa Shahada ya Masuala ya Kilimobiashara, Uchumi na Usimamizi wa tasnia ya chakula.

Alipoingilia shughuli za kilimo, mnamo 2017, alikuwa mwaka wa pili JKUAT. Boniface anasema alianza kwa upanzi wa miche ya maparachichi, ya kupandikiza, maarufu kama ‘grafted avocados’ eneo la Mutira, Kaunti ya Kirinyaga.

Akiwa limbukeni katika shughuli hiyo, Boniface anaiambia ‘Taifa Leo’ kwamba majaribio kadhaa yaligonga mwamba. “Miche niliyopandikiza haikufua dafu, mara kadhaa. Nililazimika kurejea uwanjani, kufanya utafiti wa kina namna ya kupandikiza,” anasema.

Ni kupitia tafiti zake ambapo alielekezwa kwa afisa mmoja wa kilimo Kaunti ya Kirinyaga, aliyempevusha na kumnoa makali.

Kwa mtaji mwingine, Sh2, 000 kijana Boniface alirejea kwenye uga wa kupandikiza miche ya maparachichi aina ya Hass, shughuli ambayo imegeuka kuwa kilimobiashara kinachomuingizia mapato ya kuridhisha.

Ikizingatiwa kuwa alikuwa chuoni, kizingiti kikuu kilikuwa namna ya kuendeleza azma yake kuwekeza katika sekta ya kilimo. “Wakati ambao ningepatikana ilikuwa wikendi na likizo pekee,” Boniface anaelezea, akisema gharama ya usafiri kutoka eneo la Juja, Thika ilipo JKUAT hadi Kirinyaga kila wikendi ilikuwa ghali.

Hata hivyo, mama yake anayemtaja kuwa nguzo kuu katika kufanikisha maazimio yake, alimfaa kwa kiasi kikubwa kumtunzia miche wakati hangeweza kusafiri nyumbani na pia kumpiga jeki kifedha, kando na kumlipia karo chuoni.

Anasema eneo anakotoka, wakulima wengi wangali wametekwa na ukuzaji wa maparachichi ya kienyeji, na ambayo kiwango chake cha uzalishaji matunda ni cha chini mno kikilinganishwa na yaliyoimarishwa, yaani yale ya kupandikiza.

Isitoshe, soko la avokado za zamani ni duni mno, jambo analosema linarejesha nyuma wakulima wake kimapato.

Akitumia mfano wa babake, Boniface anasema alimsaidia kuimarishaji kilimo cha maparachichi. “Kabla atambue manufaa ya avokado zilizoimarishwa, alikuwa akiuza gunia la matunda 400 ya kienyeji kati ya Sh500 – 1, 000. Hiyo ni hasara, ikilinganishwa na gharama ya kuyakuza,” anasema.

“Nilitangulia kuimarisha yaliyoko nyumbani, na ambayo mwaka uliopita tulianza kufanya mavuno,” anadokeza, akisema yalimgharimu Sh500 pekee.

Aidha, kijana huyo amekuwa wa manufaa chungu nzima kwa wakulima wa maparachichi eneo la Mutira, kupitia kiunga chake cha ukuzaji wa miche, maarufu kama G_smart farm.

Isitoshe, Boniface, 24, anafichua kwamba ana kipande cha shamba chenye ukubwa wa nusu ekari kilichosheheni maparachichi aina ya Hass na ambayo mwaka ujao anatarajia kuanza kuvuna matunda.

Aghalibu, wengi hupanda miche ya miti ya matunda msimu wa mvua. Wakati wa mahojiano, Bonface alisema kiunga chake, G_smart farm, hakikosi kumuingizia zaidi ya Sh140, 000 kila msimu wa mvua.

“Idadi ya chini ya mauzo ya miche ninayofanya ni 1, 000, kila mche nikiuza zaidi ya Sh150. Gharama ya kupandikiza na kutunza kiwango hicho cha miche ni Sh10, 000 pekee,” akasema.

Mbali na maparachichi, mkulima huyo mchanga pia hupandikiza na kutunza miche ya macadamia na kahawa.

Kulingana na James Macharia, mtaalamu, ufanikishaji wa kiunga cha miche unategemea kuwapo kwa maji safi na udongo ulioafikia vigezo faafu. “Miche yoyote ile inahitaji matunzo ya hali ya juu. Kiunga kiwe na udongo bora, wenye rutuba na maji safi,” Macharia anashauri.

Mdau huyo pia anasema ni muhimu kiwe katika mazingira salama, dhidi ya wanyama kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku. “Ndege pia ni waharibifu kwa mimea michanga, hakikisha umeweka mikakati bora kuwatimua,” anahimiza.

Ili kufanikisha kilimo cha maparachichi, ni muhimu mkulima awe na kiini cha maji ya kutosha. Mfumo wa unyunyiziaji maji mimea na mashamba kwa mifereji, unasifiwa kwa kuhakikisha taifa licha mazao ya kutosha.

Avokado moja ya Hass kulingana na Boniface, hususan ya kuuza nje ya nchi haipungui Sh10.

Kijana huyo alifuzu chuoni 2019, na ikiwa kuna hatua anayosifia ni kuingilia kilimo. Anasema kwa sasa anafanya shughuli za kilimo kikamilifu. “Nilianza kuandaa afisi yangu ya kazi nikiwa chuoni. Vikwazo vya kutafuta ajira niliviondokea kwa sababu ninaridhia kilimo,” anafafanua, akieleza kwamba taaluma aliyosomea imemfaa pakubwa.

Ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana nchini ni donda ndugu na ambalo linaendelea kuwahangaisha.

“Tangu nifuzu kwa Shahada ya Masuala ya Uchumi na Biashara, miaka minne iliyopita, jitihada zangu kupata kazi zimegonga mwamba. Ni muhimu sisi kama vijana tutathmini namna ya kujiajiri katika sekta ya kilimo na biashara,” Michael Muriuki anasema, akidokeza kwamba kwa sasa amewekeza katika biashara.

Kikwazo kinachozingira vijana nchini, ni ukosefu wa fedha, mtaji kuanzisha maazimio yao.