Makala

ULANGUZI WA BINADAMU: Waziri Echesa taabani

January 4th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Ijumaa iliamuru wasichana wanane kutoka Pakistan walioruhusiwa kuingia nchini na Waziri wa Utamaduni na Michezo Bw Rashid Echesa (pichani juu) kushiriki katika densi za kitamaduni, wazuiliwe katika chumba maalum.

Hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot alitoa agizo hilo baada ya kukabidhiwa barua iliyokuwa imetiwa saini na Bw Echesa.

Wakili Evans Ondieki anayewawakilisha wasichana hao pamoja na mwenye kilabu cha Bella Bella, mtaani Parklands, Nairobi Bw Safendra Kumar Sonwani alimkabidhi hakimu nakala za pasi hizo maalum na riziti za Sh45,000 ambazo kila mmoja alilipa kupewa pasi hizo.

Bw Ondieki alisema tangu wasichana hao walipotiwa nguvuni Desemba 31, 2018 siku ile waliingia nchini , “hawajaoga au kubadilisha nguo.”

Akasema, “Naomba hii mahakama ionyeshe utu na kuwaachilia wasichana hawa wanane. Tangu watiwe nguvuni hawajabadilisha nguo za ndani na za juu wala kuoga.”

Aliongeza kusema, “Naomba korti itilie maanani hawa ni wanawake na sheria za usafi huwataka kukaa wakiwa safi.”

Baadhi ya wasichana kutoka Pakistan ambao Waziri Echesa anadaiwa kuwalangua. Picha/ Richard Munguti

Bw Ondieki alisema mmiliki wa shirika moja lilisilo la kiserikali lijulikanalo kama Blue Heart, Bw Nadeem Khan, yuko tayari kuwapa makao na polisi wako huru kuwatembelea pale.

“Naamuru wasichana hawa wanane ambao ni mashahidi katika kesi ya ulanguzi wa binadamu wazuiliwe katika makazi maalum ambapo polisi kutoka kitengo cha uhalifu wa kimataifa wanaweza kuwafikia wakati wowote,” aliamuru Bw Cheruiyot.

Hakimu aliongeza kusema, “Ni Bw Khan tu pamoja na polisi wanaruhusiwa kuwasiliana na wasichana hawa wanane.”

Korti iliagiza wasichana hao wafikishwe kortini tena mnamo Januari 8, 2019.

Na wakati huo huo mahakama iliamuru mwenye kilabu cha Bella Bella azuiliwe hadi Januari 8, 2019 polisi wathibitishe ikiwa pasi maalum wasichana hao walizokuwa nazo ni halali au bandia.

Wakili Evans Ondieki (kulia) na Nadeem Khan wakiwa nje ya mahakama kuu ya Milimani, Nairobi Januari 4, 2019. Picha/ Richard Munguti

 

Bw Sonwani pamoja na meneja wake Bw Mika Osicharo wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Parklands.

Ombi la kuwatia washukiwa hao wawili ndani liliwasilishwa na kiongozi wa mashtaka Bi Annette Wangia.

Bi Wangia aliomba mahakama iwazuilie wawili hao ndipo maafisa wa polisi wakamilishe uchunguzi kubaini ikiwa wasichana hao wanane wako na vibali vya kuwaruhusu kuingia nchini.

“Naomba mahakama iwazuilie Mabw Sonwani na Osicharo kwa muda wa siku tano Polisi wabaini ikiwa wasichana waliokamatwa Januari 1, 2019 katika kilabu cha Balle Balle walikuwa na hati rasmi za kuwaruhusu kuingia nchini,” alisema Bi Wangia.

Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na wakili Evans Ondieki aliyesema kuwa wasichana hao walipewa pasi spesheli na Waziri wa Utamaduni na Michezo Bw Rashid Echesa.

Safendra Kumar Sonwani (kulia) na Mika Osicharo wakiwa kizimbani. Picha/ Richard Munguti

“Wasichana hawa walikubaliwa kuingia nchini na Bw Echesa. Nashangaa sababu polisi wamewakamata Mabw Sonwani na Osicho kwa madai ya kuwalangua wasichana hao,” alisema Bw Ondieki huku akimkabidhi hakimu nakala za pasi maalum walizopewa wasichana hao.

Alisema muda wa pasi hizo utaisha Januari 18, 2019.

“Ikiwa idara moja ya serikali haijui ile nyingine vile inafanya basi inamaanisha serikali haitekelezi kazi pamoja,” alisema Bw Ondieki.

Mahakama iliombwa iwazuilie wasichana hao katika chumba maalum kwa vile ni mashahidi wa kulindwa.

“Ikiwa pasi hizi maalum zitabainika ni feki basi wasichana hawa na Mabw Sonwani na Osichori watashtakiwa kwa makosa ya ulanguzi wa binadamu,” alisema Bw Wangia.