Kimataifa

Ulaya sasa yahofia kurejea kwa Trump mamlakani Amerika

January 16th, 2024 2 min read

BRUSSELS, UBELGIJI

NA MASHIRIKA

ALIYEKUWA Rais wa Amerika Donald Trump anatishia mataifa mengi barani Uropa kwa kuwania tena urais Amerika.

Kulingana na mkuu wa soko la ndani la Muungano wa Ulaya, Thierry Breton, Trump alimwambia Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen mwaka wa 2020 kwamba “ikiwa Ulaya itashambuliwa, hatutakuja kuwasaidia na kuiunga mkono.”

Matamshi ya Breton wakati wa hafla katika Bunge la Ulaya yalijiri wiki moja kabla ya vikao vya Iowa na kuanza kwa kura katika mchujo wa urais wa chama cha Republican nchini Marekani, ambao Trump alishinda Jumatatu Januari 15, 2024 usiku.

Pia ziliambatana na pendekezo la Breton la Hazina ya €100bn ili kuimarisha utengenezaji wa risasi – jambo ambalo limekosolewa vikali.

Maafisa na wanadiplomasia wengi wa Umoja wa Ulaya waliiambia shirika moja la habari za kimataifa kwamba kurejea kwa Trump kuwania urais kunaleta tumbo joto wakati Umoja wa Ulaya ukijaribu kujenga uwezo wake wa ulinzi nje ya muungano wa NATO unaoongozwa na Marekani.

Si siri kuwa nchi nyingi zimekumbwa na upungufu wa risasi hasa katika nchi wanachama wa NATO kwa sababu nchi za magharibi zinatoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine.

Ikiwa Trump kweli alitoa maoni hayo au la si muhimu kwa maafisa wa Uropa.

Maoni ya Trump kuhusu nafasi ya kihistoria ya Amerika katika usalama wa Ulaya yanajulikana.

Wakati akiwa uongozini, Trump alizungumza mara kwa mara kuhusu kufadhili NATO huku pia akiwapongeza marais waliotawala kimabavu, akiwemo Vladimir Putin wa Urusi, ambao wanachukuliwa kuwa maadui wa muungano huo wa kijeshi.

Ukumbusho kwamba Trump ana nia hiyo na ukweli kwamba hivi karibuni anaweza kurejea White House, husababisha wasiwasi na uchungu wa kweli jijini Brussels, nchini Belgium.

Katika jiji la Brussels, ndiko kuna makoa makuu ya NATO.

Uchaguzi wa Amerika unatarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu na tayari joto linaonekana kuanza kupanda, ushindani ukitarajiwa kuwa kati ya Rais Joe Biden na Trump ambao walipambana miaka minne iliyopita.

Katika uchaguzi mkuu uliofanywa mwaka wa 2020, Trump alishindwa na Joe Biden na hivyo kuingia katika historia ya kuhudumu katika wadhifa wa urais kwa awamu moja pekee.

Uchunguzi ndani ya chama cha Republican zinaashiria kiongozi huyo (Trump) ataibuka mshindi dhidi ya wapinzani wake katika maeneo ya Magharibi mwa Amerika.