HabariMakala

Ulevi wa wanawake wachambuliwa

July 24th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

SIKU hizi ni kawaida kuwaona wanawake vilabuni wakilewa, wengine hata wakiwa na uwezo wa kubugia viwango vya juu kuwaliko wanaume.

Swali ni je; katika uraibu huu wa ulevi, wanawake watajiweka salama namna gani?

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Bomet Naomi Ichami, wanawake wamezingatiwa katika sheria kama walio na hatari kuu ndani ya baa wakilewa.

“Kando na kuwa na hela, wao huwa na bidhaa na vifaa vya thamani kama simu na vibeti. Usisahahu kuwa wako na maumbile ya thamani katika hatari ya giza,” anasema Ichami.

Anasema kuwa ni heri kila mwanamke ambaye hujua hulewa ajiwekee mikakati yake ya kujiweka salama ndani ya mabaa na katika mikondo ya kurejea nyumbani kwao.

Hali halisi iko namna gani?

Ndipo tunazama ndani ya baa na kupata wahudumu wawili ambao ni Mercy na Anne na kuwauliza swali: Ni vipi mwanamke anaweza akajiweka salama ndani ya baa?

Mercy anasema kuwa uamuzi wa kina wa kujiingiza katika ulevi sio wa ajabu kwa mwanamke.

“Wanawake wanalewa. Sio siri tena. Nimewauzia si mara moja na inaonekana jinsi maisha yasongavyo, ni kama huu ulevi wa wanawake unaendelea kugeuka kuwa utamaduni… Inategemea nia ya mwanamke kuingia kwa baa ilikuwa gani,” anajibu.

Anasema kuwa katika huduma yake ya miaka mitano sasa ndani ya mabaa tofauti, amegundua kuwa wanawake hulewa kwa misingi tofauti.

“Kuna baadhi ambao huingia katika baa kusaka raha kiasi tu. Hawa ni wale wanawake ambao wamejiweza. Hawa huwa wanakunywa pombe kidogo katika muda ambao mamlaka za kiutawala zimeweka. Wakishamaliza, huondoka bila kuzua lolote lisilo la kawaida. Ni mteja ameingia akiwa peke yake au wakiwa kundi la urafiki, wanaagiza, wanabugia, wanalipa bili na wanaondoka,” anasema akiongeza kuwa hao tayari wamejishauri jinsi ya kuwa salama ndani ya ulevi.

Anasema kuwa kuwa kuna wengine ambao hawana msimamo wa ni kwa nini wako kwa baa.

‘Hawa ni wale ambao wanaonekana kukosa mstakabali mwafaka wa maisha yao. Ni kama hawana la kufanya katika maisha nje ya baa na huja tu wakiwa hawana leno linalojulikana. Watalewa, wakorofishane, wazidiwe na ulevi, watumiwe visivyo na wanaume bila mpangilio wowote na hatimaye wawe katika kila aina ya hatari,” asema.

Anasema kuwa ushauri wake kwa hawa wa kiwango hicho cha ulevi ni wakae mbali na baa, wajaribu kujaza masaa yao na kazi nyingine nje ya baa.

Kuna wengine ambao nia yao kuu ni kuibia wanaume.

‘Hawa huwa tunawatambua na jinsi kila mwanamume ambaye hutangamana naye hulia kupotea kwa aidha simu ama pesa…Hawa ni sawa na makahaba. Watafanya juu chini kunasa mwanamume aliye na pesa na aliyefungua roho yake kwa hisia za mahaba na katika harakati za kupendana na kuchumbiana kiharamu, mwanamke huyu anavuna kwenye hakupanda,” anasema.

Anasema kuwa hao wanawake huishia kutandikwa vibaya wakati wamenaswa au wanaishia kuingizwa ndani ya jela kimchezomchezo tu.

Ushauri wake kwao? “Jua kila kazi iko na mshahara wake na vya haramu huzawadiwa vya ukatili.”

Bi Anne anasema kuwa kuna wale nao wanawake wachanga ambao huingia ndani ya mabaa kufanya majaribio ya kimaisha.

“Hawa ni wa orodha ya wanafunzi na ambao huingia ndani ya mabaa kusaka raha na kujipa ufahamu wa uhuru halisi nje ya uthibiti wa wazazi. Hawa ndio huwa katika hatari kuu ya kimaisha kwa kuwa huishia kutangamana na wema na wabaya, wanasajiliwa kwa mengi ambayo hawakujua yamo ndani ya mabaa na hatimaye maisha yao yanawaendea visivyo,” anasema.

Anayataja hayo mengine ambayo hayajulikani yamo ndani ya mabaa kama utumizi wa mihadarati, ngono kiholela na utekaji nyara kwa minajiri ya ujambazi na hatimaye hata kuambukizwa magonjwa yasiyo na suluhu la kimatibabu.

Kwa hao anawaonya kuwa “ingia kwa baa ikiwa unajielewa na unajifahamu kuwa huwezi ukashawishika kwa urahisi kutenda yale ambayo hujajipangia mwenyewe.”

Lakini anatoa tahadhari kwa wanawake wote kwa ujumla: “Kaa nje ya baa ikiwa wewe sio mwajiriwa katika baa. Kaa nje ya baa ikiwa kazi kubwa yako unasaka hapa ni kulewa. Hakuna kitu nimekuja kuona kina madhara makuu kuliko ulevi wa wanawake.”

Anathubutu kusema “pombe haikuundiwa wanawake.”

“Uevi sio uraibu mwafaka wa mwanamke. Tuachie wanaume ulevi kwa kuwa hata wakati mambo yamewaendea vibaya sana ndani ya ulevi, huwa wako na ujasiri wa kimaisha wa kujinyanyua na kwendelea mbele na maisha,” anasema.

Anasema kuwa kwa sasa, usalama wa mwanamke ndani ya ulevi ni kukaa mbali na ulevi.