Makala

Ulijua kunywa maji kupindukia kunasababisha ugonjwa unaojulikana kama Psychogenic Polydipsia?

March 25th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

MAJI ni uhai, na ni kiungo muhimu sana maishani kwa binadamu, wanyama na mimea. 

Tumefunzwa kuanzia tukiwa wachanga kwamba unywaji maji ndio nguzo ya kuishi vyema.

Mtu anashauriwa kunywa aghalabu lita tatu za maji kila siku.

Hata hivyo, ulijua kuwa kuyanywa kupindukia kuna athari zake mwilini?

Wanasayansi na wataalamu wanahoji ukinywa maji kupindukia kiwango kinachohitajika kunasababisha maradhi yanayojulikana kama Psychogenic Polydipsia.

Richard Oduor, Profesa tajika wa Masuala ya Molecular Biology, Genetic Engineering, Drug Discovery, and Forensic Science, anaainisha zaidi kuhusu athari za kunywa maji kupindukia.

Mhadhiri huyu wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU), anatoa changamoto kwa wanaokunywa maji kupita kiasi akisema si bora kiafya.

“Maji tunayosema ni uhai, yakinywewa kwa wingi yatasababisha madhara mwilini,” Prof Oduor anasema.

Anaongeza, “Ni ukumbusho; kila kitu kinachoonekana kuwa na thamani na manufaa, hakikosi ubaya wake”.

Akionekana kukaza spana katika karakana kazini, Msomi huyu ambaye ni Mtafiti gwiji katika Masuala ya Bayoteknolojia kwenye Kilimo anatahadharisha unywaji wa maji kupindukia akifichua maradhi yanayotokana na kiungo hicho muhimu.

“Ndio, unywaji maji kupita kiwango hitajika unasababisha ugonjwa unaojulikana kama Psychogenic Polydipsia,” Prof Oduor anaonya.

Psychogenic Polydipsia ni maradhi yanayotokana na mazoea ya kunywa maji kupita kiasi, bila kuwepo kwa stimuli za Kibayolojia za kunywa.

Aghalabu, husababishwa na matatizo ya kiakili.

Richard Oduor, Profesa tajika wa Masuala ya Molecular Biology, Genetic Engineering, Drug Discovery, and Forensic Science. PICHA|SAMMY WAWERU

“Hali hiyo inatokana na kero ya kunywa maji kupindukia. Maji ambayo tunasema ni uhai,” Prof Oduor asema.

Msomi huyu alitoa kauli hiyo kupitia mahojiano ya kipekee na Taifa Dijitali, hasa akirejelea mjadala tata kuhusu suala la bidhaa za GMO.

Usambazaji wa bidhaa za GMO – Zilizoimarishwa kupitia msimbojeni, ulisitishwa kwa muda na mahakama baada ya Rais William Ruto mwaka wa 2022 kuondoa marufuku ya miaka 10 iliyokuwepo.

GMO, bunifu na teknolojia ya kisasa (Bayoteknolojia) kuendeleza shughuli za kilimo ilizinduliwa nchini zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Prof Oduor anahimiza Wakenya kukumbatia mfumo wa Bayoteknolojia, akihoji utasaidia kuangazia kero ya njaa, uhaba na usalama wa chakula Kenya.

Msimbojeni (DNA), Mwanasayansi huyu anasema unaweza kuboreshwa ili kuibuka na mmea au kitu kilichoimarishwa chenye uhai.

“GMO, imetumia teknolojia ya kuhamisha au kusafirisha jeni (genes) kutoka kwa kitu kimoja chenye uhai na kuipeleka kwa kingine kwa lengo la kukiboresha,” Prof Oduor anafafanua.

Huku mjadala wa Bayoteknolojia ukionekana kuzua tumbojoto hasa kwa wakosoaji wake, Mtaalamu huyu anafananisha teknolojia inayotumika na kuwepo kwa kisu.

Kisu, ni teknolojia kurahisisha kukatakata mboga ila kinaweza kutumika kutekeleza uhalifu – kuua mtu, na mtuhumiwa atajipata akiandamwa na polisi na mahakama, ili kukumbana na makali ya sheria.

Hivyo, Prof Oduor anasema mfumo wa Bayoteknolojia una kanuni na sheria zake – kupitia asasi (National Biosafety Authority) zilizotwikwa kutathmini teknolojia, sawa na mhalifu kwa njia ya kisu.