Makala

ULIMBWENDE: Jinsi unavyoweza kuchagua manukato yanayokufaa

July 30th, 2020 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

KUNA manukato aina mbalimbali madukani, lakini sio yote mazuri kwa kila mtu.

Ni muhimu kuchagua manukato ambayo yatamfaa mtumiaji.

Pafyumu unapoinusa, inagawanyika mara tatu, yaani kile unachokisikia na ‘ukali’ wake unavyotofautiana.

Hiyo ndiyo sababu kuna manukato ambayo ukinunua ukajipulizia au kujirashia yanakuwa kama harufu inabadilika kadri inavyosikika inapojichanganya na hewa. Wakati baadhi ya manukato hupoteza mvuto kabisa kadri muda unavyoenda, mengine huendelea kupendeza kadri siku zinavyosonga.

Kuna manukato yanayopoteza mvuto haraka, kuna ambayo utayasikia baada ya harufu ya mwanzo kupotea na kuna yale ambayo yatabaki muda mrefu.

Pafyumu hugawanywa kulingana na aina za harufu ambazo kwa upande mwingine zinaamua ipi ni ya kiume na ipi ya kike.

Aina za harufu hutofautiana kutokana na viungo vilivyotumika kutengeneza.

Jinsi ya kuchagua pafyumu au manukato yanayokufaa

Usiwe na haraka kununua manukato. Chukua muda kutafuta yalio mazuri. Chagua harufu unayojisikia vizuri ukiinusa. Ni vema uchague manukato yanayokupa hisia nzuri, yanayokufanya ujipende na ujisikie vizuri.

Zingatia jinsi ulivyo

Hapa ni vyema ukajijua wewe ni mtu wa aina gani na unapenda kuonekana vipi. Kama wewe ni mtu mnyamavu mwenye kupenda mambo ya kimyakimya na unayetaka utulivu sana, basi chagua harufu nyepesi au laini mfano harufu za vanilla. Na iwapo wewe ni mtu unayependa kuonekana na kusababisha watu wageuze shingo zao unapopita, basi pia chagua harufu itakayokutambulisha kuwa unapita au umepita pahala hapa au pale.

Jaribu kunusa manukato kwanza kabla hujanunua

Hii itakuhakikishia kwamba unanunua kitu unachokitaka. Kama hujayanusa vyema yanaweza yakawa manukato yanayobadilika harufu mwishoni hivyo kuwa kikwazo kwako na wengine watakaoipata harufu ya manukato yako.

Shirikisha mtu mwingine katika kuchagua harufu nzuri

Hii itasaidia kuchagua manukato mazuri ambayo hayatakwaza watu watakaokuzunguka ama kiafya (alergy ya harufu kali) au kihisia.