Makala

ULIMBWENDE: Kuzuia kukauka kwa midomo

November 18th, 2020 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

TATIZO kubwa tunalopitia msimu wa baridi ni midomo kavu iliyokauka na kukaukiana.

Wakati mwingine inakatika na kuwa na vidonda.

Ili kuzuia hali hii, vipo vitu unavyopaswa kuvifanya.

Kabla ya kuendelea na njia za asilia ni muhimu uelewe kuwa kama unahitaji ubora wa urembo wako unatakiwa kunywa maji ya kutosha. Hivyo basi, kunywa maji angalau glasi nane kwa siku. Pia ni muhimu ufahamu sababu za ukavu wa mdomo.

  • kuramba midomo yako – lips – kwa kutumia ulimi; mate yana uwezo mkubwa wa kukausha midomo
  • kuathiriwa na mwanga wa jua
  • kuvuta sigara na kunywa pombe
  • vichubua ngozi vinavyopatikana mfano kwenye dawa za meno
  • uzio “allergies”
  • baadhi ya dawa

Cocoa butter

Hapa unaweza kutumia Cocoa butter au Shea butter. Chukua Cocoa butter au Shea butter; weka kwenye lips zako na lala nayo. Fanya hivyo kila siku hadi uone matokeo.

Mshubiri (Aloe vera)

Mshubiri huwa na virutubisho muhimu vinavyohitajika kwa ngozi yako. Utahitaji jani moja la Aloe vera. Chukua Aloe vera kisha kata jani lake vipande vipande utoe jeli yake kisha upake kwenye lips. Unaweza kulala nayo. Tumia hadi uone matokeo.

Tahadhari: Aloe vera ni chungu, kuwa muangalifu unapoitumia.

Mafuta ya Asili

Mafuta ya asili kama vile:

Mafuta ya nazi

Jojoba oil

Mafuta ya mzeituni

Mafuta ya parachichi

Mafuta ya mnyonyo (castor oil)

Mafuta ya lozi (almond)

Mafuta yote hayo yana uwezo wa kukuondolea ukavu wa lips. Chukua aina moja ya mafuta, paka kwenye lips zako. Rudia hadi uone mabadiliko mazuri.

Mafuta ya nazi na sukari

Chukua sukari kiasi kijiko kimoja na mafuta ya nazi vijiko vitatu. Changanya ili upate mchanganyiko mzuri wa kuweka kwenye lips. Acha kisha baada ya dakika 20 osha kwa maji ya kawaida. Rudia hadi uone matokeo.

Majani ya waridi “rose” na maziwa fresh

Chukua majani ya waridi kiasi uyachanganye na maziwa kisha saga upate mchanganyiko mzito. Weka kwenye lips mchanganyiko huo kwa dakika 20. Osha kwa maji ya kawaida. Rudia hadi uone matokeo bora.

Tango

Tango lina virutubisho vya kutosha. Unachotakiwa kufanya ni kuchukua tango moja ulikate vipande vidogovidogo vya umbo mduara halafu uviweke kwenye lips zako. Baada ya dakika 30 osha.

Acha kurambaramba lips zako kwa ulimi kwa sababu mate yanasababisha ukavu zaidi. Ni muhimu unywe maji ya kutosha kila siku.