Makala

ULIMBWENDE: Jinsi ya kuifanya mikono, viganja na vidole kuwa laini

September 17th, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

JAPO hatua ya kunywa maji kwa wingi ili kuwa na ngozi laini ni nzuri, unaweza pia kutumia njia zifuatazo iwapo unataka mikono na viganja kuwa laini.

Weka sabuni ya maji ya kuoshea mikono. Baada ya kuosha mikono, kausha mikono yako vizuri.

Chukua bakuli, weka chumvi vijiko viwili.

Ongeza vijiko viwili vya mafuta ya mizeituni.

Kisha weka mchanganyiko huo kwenye viganja vyako kisha sugua polepole.

Sugua ndani na nje ya viganja na ndani ya vidole na kucha.

Osha kwa maji ya vuguvugu kisha kausha mikono kwa kutumia taulo kavu.

Malizia kwa kupaka losheni yako kama kawaida.

Njia ya pili

Osha mikono na maji yenye uvuguvugu huku ukitumia sabuni ili kuondoa mafuta na bakteria.

Kausha mikono kwa taulo kavu na safi.

Chukua sukari vijiko viwili na mafuta ya mizeituni pia vijiko viwili. Paka mikononi. Sugua mikono yote kwa pamoja ndani na nje kwa kutumia mchanganyiko huo.

Osha mikono kwa maji ya uvuguvugu

Kausha mikono yako kisha upake rose water. Unaweza pia kutumia sunflower oil au mafuta ya nazi.

Mambo muhimu ya kuzingatia

Usifanye mara moja ukategemea matokeo ya kudumu.

Paka losheni kabla ya kulala.

Vaa glavu wakati unafanya kazi kama kuosha vyombo.

Usiache mikono kwenye maji baridi kwa muda mrefu kwa sababu kufanya hivyo, kunachangia kuondoka kwa mafuta na unyevu wa asili mikononi.