Makala

ULIMBWENDE: Jinsi ya kuondoa madoa meusi

September 12th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MADOA meusi (black spots) usoni ni tatizo ambalo linawasumbua wanawake wengi sana na husababisha mtu kutokujiamini na mara nyingine kujidharau, na kushindwa kukaa bila kutumia vipodozi.

Hili tatizo husabaishwa na vitu tofauti kama vile;

Hyperpigmentation

Hili tatizo linatokea pale ngozi inapoharibiwa katika eneo fulani, hivyo husababisha ngozi kutengeneza ‘melanin’ nyingi na kusababisha eneo hilo kuonekana nyeusi kuliko sehemu zingine.

Homoni

Homoni zinapozalishwa katika kiwango kisicho sahihi katika mwili; matokeo huwa ni Hormonal imbalances. Hali hii husababisha madoa meusi usoni. Hili linaweza tokea wakati wa ujauzito, kwa watu wanaotumia tembe kama mpango wa uzazi (control pills) na pia kwa mwanamke anapoingia katika kipindi cha ukomo wa kuzaa (menopause).

Kukaa juani kwa muda mrefu

Kunasababisha mwili kuanza kutengeneza ‘melanin’ kwa wingi ili kuzuia kuharibiwa kwa ngozi na mionzi ya jua. Na kadri mwili ufanyavyo hivyo ndivyo mtu huanza kuwa na madoa meusi usoni.

Chunusi

Pia weusi hutokea kwa watu ambao wana tatizo la chunusi. Wengi wenye chunusi huwa na tabia ya kutumbua chunusi na kwa kufanya hivyo, makovu yanapona huku yakiacha weusi usoni. Mara nyingi haya madoa meusi yanapotea baada ya muda fulani kupita, lakini muda mwingine inaweza ikawa ni vigumu kupotea yenyewe kutegemea na aina ya chunusi.

JINSI YA KUONDOA MADOA MEUSI UKIWA NYUMBANI

Tumia juisi ya mshubiri

Paka Aloe vera katika sehemu yenye madoa meusi mara mbili kwa siku. Fanya hivi kwa wiki kadhaa ili upate kuona mabadiliko.

Asali na sukari

Changanya asali na sukari hii ya kawaida na ujikande mara mbili kwa wiki ili kuondoa ngozi zilizokufa na kufanya ngozi mpya na hivyo kuondoa madoa meusi.

Tumia matunda ambayo yamesheheni vitamini C na E

Matunda kama machungwa yana vitamini C ambayo ni Anti-oxidant na pia hupunguza melanin isitengenezwe kwa wingi na hivyo kufanya ngozi isiwe na madoa meusi.

Tumia krimu inayaosaidia ngozi kujilinda dhidi ya mionzi ya jua

Hizi krimu huzuia mionzi ya jua ambayo ni chanzo kimojawapo cha madoa meusi usoni. Hakikisha unatumia krimu hizi kabla ya kutoka nje.

Pia ukiona madoa yako hayatoki, unaweza ukamwona mtaalam wa ngozi kwa ajili ya ushauri na matibabu zaidi.