Makala

ULIMBWENDE: Jinsi ya kuvaa viatu mbalimbali

November 6th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

VIATU ni vitu vinavyovaliwa na ambavyo ni kinga kwa ajili ya kuhifadhi miguu.

Viatu huongeza urembo na nakshi kwa mvaaji.

Viatu vipo vya aina mbalimbali na vinavaliwa kulingana na mahali na mavazi yanayoambatana navyo sema pengine kwa rangi au hata umbo.

Viatu vya ngozi vya kufunika

Viatu vya kufunika vipo virefu sana, vyenye urefu wa wastani na vifupi kabisa. Mara nyingine haviwi vya ngozi kabisa bali ni kama vina plastiki na pia vingine huwa na uwazi japo mdogo kwa mbele.

Viatu virefu hupendeza zaidi kuvaliwa kwenye sherehe na kanisani. Unaweza kuvaa kazini kama kazi yako haikulazimu kutembeatembea maana vitachosha miguu yako.

 

Viatu vyenye visigino virefu aina ya stiletto katika mojawapo ya maduka jijini Nairobi katika hii picha ya Desemba 13, 2012. Picha/ Maktaba

Viatu vyenye urefu wa wastani mvaaji anaweza kuvaa popote ama iwe kazini, kanisani au katika sherehe.

Viatu vya chini kabisa vinakuwa vyenye matumizi zaidi wakati una matembezi mengi. Havifai sana kuvaliwa kwenye sherehe za usiku hasa kama unavaa nguo maalumu ya usiku. Vinafaa sana kwa mjamzito hasa katika miezi ya mwisho.

Viatu vya wazi virefu

Viatu hivi vipo vya aina mbili, vyenye rangi za mng’ao na ambavyo ni mahususi kwa sherehe za usiku na vyenye rangi ngumu ambavyo waweza kuvaa kazini au kanisani.

Viatu hivi vinapendeza kuvaliwa na nguo yoyote ila ikiwa ya urefu wa wastani ni nzuri zaidi maana huwezesha kuonekana urembo na uzuri wote wa kiatu.

Viatu hivi vinakuja katika mitindo mbalimbali na unachagua ule ambao wewe unaupendelea zaidi. Mfano, vyenye visigino vyembamba, visigino vinene au aina ya ‘wedges’.

Viatu vya wazi vifupi

Viatu hivi ni vizuri kwa sababu vinawezesha miguu kupumua na ku-relax. Viatu hivi vipo vya aina tofauti tofauti na vinafaa sana kuvaliwa kwa matembezi ya jioni, wakati wa safari ndefu, wakati ukiwa na mizunguko mingi na pia hata kazini au kanisani pale unapokuwa umevaa nguo za kawaida. Havivutii sana kuvaliwa na suti au nguo ya usiku. Pia mara nyingi viatu vya chini hupendezea kuvaliwa na nguo ndefu na viatu virefu hupendeza zaidi kwa nguo yenye urefu wa wastani.

Viatu vya muda maalumu

Hivi ni viatu ambavyo vinavaliwa wakati wa kazi maalumu kama wakati wa kazi za mashambani, wakati wa michezo au wakati wa baridi kali.

Ni vyema na inapendeza kama una uwezo uwe na viatu vya aina mbalimbali angalau aina tatu. Mfano, viatu vyeusi vya urefu wa wastani, viatu vya usiku vya wazi, viatu vya chini vya kufunika na vya wazi.