Makala

ULIMBWENDE: Mafuta ya nazi na manufaa yake mwilini

May 7th, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MAFUTA ya nazi ni mazuri kama yatatumika jinsi ipasavyo kwani yana uwezo wa kukufanya uonekana mrembo mwenye ngozi ya kuvutia ajabu!

Kuondoa makeup

Mafuta ya nazi yanaweza pia kutumika kuondoa makeup usoni. Mtumiaji anashauriwa kuitoa makeup kabla ya kuenda kulala. Katika kufanya kazi hiyo, mafuta ya nazi yanatumika hivi:

– chukua pamba safi chovya kwenye mafuta ya nazi
– futa uso wako taratibu kwa kutumia pamba iliyo na mafuta ya nazi
– baada ya kufuta tumia cleanser au nawa uso wako vizuri kwa sabuni

Kulainisha ngozi

Mafuta ya nazi pia hutumika kama kilainishi cha ngozi yako hasa kwa

– kuondoa magaga kwenye nyayo za miguu
– kuzuia mipasuko ya nyayo za miguu
– kupunguza hali ya kukauka kwa ngozi ya mikononi

Hivyo, mafuta ya nazi yanasaidia kwa kiasi kikubwa sana kulainisha ngozi na kuipa afya nzuri.

Kuondoa seli zilizokufa

Mafuta ya nazi husaidia kuondoa ngozi iliyoharibika katika mwili. Mtumiaji anahitajika tu

– kuchukua mafuta ya nazi, sukari na chumvi na kuchanganya ili kupata mchanganyiko mmoja kisha kupaka katika mwili mzima.
– kufanya masaji kwa mchanganyiko huo na kukaa nao kwa muda kabla ya kuoga.

Bila shaka mtumiaji ataona tu mabadiliko katika ngozi yake baada ya kukamilika kwa shughuli hii.

Mi muhimu kufanya hivyo mara tatu kwa wiki au kipindi hata kirefu zaidi ya hapo.

Husaidia katika kunyoa

Wengi wetu tumezoea kutumia Shaving cream wakati wa kunyoa nywele lakini mafuta ya nazi pia yanaweza kutumika hapa badala ya shave cream, yenyewe yanasaidia kutibu vipele vinavyojitokeza baada ya kunyoa.

Kukuza nywele

Mafuta ya nazi yanatumika katika kurutubisha nywele na kufanya ziwe na nuru. Ni muhimu kupaka kwenye ngozi na pia sehemu ya nywele ambazo ni hafifu au zilizokatika.