Makala

ULIMBWENDE: Makosa ambayo baadhi ya watu hufanya wakati wa kuosha nywele

May 14th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

WENGI wetu tumekuwa tukifanya makosa kadhaa wakati wa kuosha nywele.

Baadhi yetu hatutumii muda wa kutosha kusugua ngozi ya kichwa, hatuoshi vizuri na baadhi pia hatutumii conditioner.

Kutolowesha nywele vizuri

Watu wengi hawaloweshi nywele zao vizuri kabla ya kupaka shampoo.

Ni muhimu kulowesha kila unywele kwa maji kabla ya kupaka shampoo.

Sote tunafahamu kwamba kitu chochote kikizidi kina madhara au hakitaleta matokeo mazuri. Tunatakiwa kutumia kila kitu kwa kiasi. Si kwa wingi sana na si kwa uchache sana. Hii ina maana kwamba kutumia shampoo nyingi kunaweza kukufanya usiweze kuipata nywele na kuisafisha vizuri kutokana na kuzidiwa na povu nyingi sana. Na kutumia shampoo kiasi kutafanya nywele zako zisitakate vizuri.

Pima shampoo kiganjani kwako, kiasi cha wastani kulingana na ukubwa na wingi wa nywele zako. Kwa kutumia vidole, paka shampoo kwenye nywele zako ulizozigawanya kwenye makundi manne. Paka kuanzia kwenye ngozi ya kichwa (scalp) kuja kwenye ncha ya nywele.

Watu wengi hawatumii muda wa kutosha kusugua ngozi ya kichwani. Tunatakiwa kusugua ngozi hizi kwa angalau dakika tatu.

Bila kujali urefu au aina ya nywele zako, unachotakiwa ni kusugua ngozi yako ya kichwa. Na unatakiwa kufanya hivyo kwa kutumia vidole na sio kucha kwa muda usiopungua dakika tatu.

Kutokuosha na kurudia (rinse & repeat)

Ni muhimu sana kuosha nywele na kurudia. Na hii ni muhimu zaidi kwa wale wenye nywele ndefu. Kama una nywele fupi au ndogo kabisa, si lazima kwako kuosha na kurudia. Baada ya kuwa umesugua ngozi ya kichwa kwa dakika tatu, ni muda wa kuosha nywele.

Ukishaosha, inafuata hatua ya pili ya uoshaji wa nywele. Unatumia shampoo kama kawaida.

Kwenye hatua hii utaweka msisitizo zaidi kwenye nywele zenyewe kwakuwa tayari ngozi ya kichwa ulishashughulika nayo kabla. Mara hii weka msisitizo zaidi kwenye kuosha nywele zako na hakikisha hakuna nywele inayoachwa bila kupata shampoo kuanzia kwenye mzizi mpaka kwenye ncha.

Kutokutoa shampoo vizuri kwenye nywele

Baada ya kurudia kuosha nywele kwa mara ya pili kinachofuata ni kutoa shampoo kwenye nywele.

Watu wengi hawatoi shampoo vizuri kwenye nywele, na hii huzifanya nywele kubaki na shampoo ambazo zinasababisha nywele kubaki na vitu vyeupe vyeupe na nywele pia kutosafishika vizuri.

Hivyo inasisitizwa kutumia muda na maji ya kutosha kutoa shampoo na kuhakikisha imetoka kabisa kwenye nywele ili nywele zako ziwe zimesafishika vizuri.