Makala

ULIMBWENDE: Manufaa ya viazi mbatata katika urembo

March 6th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

VIAZI kwa kawaida ni chakula chenye madini mengi muhimu kama vitamini A, C, B, na iron.

Viazi vina manufaa kwa ngozi zetu waja.

Unaweza kutumia viazi nyumbani ili kuifanya ngozi iwe nyororo.

Faida za viazi kwa ngozi

Viazi huondoa madhara ambayo yanakuwa yamesababishwa na jua na kuleta mwanga wa asili wa ngozi.

Viazi vinapunguza wekundu na matatizo ya ngozi kutokana na vipele ,makovu na chunusi.

Viazi vinafanya ngozi iwe ya rangi moja na laini.

Viazi husaidia kuondoa mikunjo kwenye uso.

Viazi huondoa weusi kwenye kwapa.

Ili kusaidia ngozi iwe na rangi moja

Utahitaji

 • Vijiko vitatu vya juisi ya viazi
 • Mafuta ya lozi vijiko viwili (almond oil)
 • Maziwa vijiko viwili

Cha kufanya

Kwenye kijibakuli changanya mahitaji au hivi vyote vinavyohitajika na upake kwenye uso bila ya kusahau shingo na sehemu zote utazohitaji.

Ache kwa muda wa nusu saa kisha osha kwa maji fufutende.

 

Kuondoa makovu na madoa

Unahitaji

 • Kipande cha kiazi
 • Sukari vijiko 2

Cha kufanya

Nyunyiza sukari kidogo kwenye kipande cha kiazi na ujisugue kwa dakika tano.

Uache mchanganyiko kwenye uso wako kwa dakika kumi, kisha osha kwa maji baridi.

 

Kuondoa weusi na madoa

Limau na viazi hutumika kama mkorogo wa asili na huondoa weusi wowote na madoa kwenye ngozi.

Unahitaji

 • Kiazi kidogo kimoja kilichopondwa
 • Vijiko vitatu vya juisi ya ndimu au limau

Cha kufanya

Ponda kiazi na weka vijiko vitatu vya juisi ya limau.

Changanya na paka kwenye makovu.

Iache kama dakika 20 mpaka 30 kisha osha vizuri na maji.

 

Kwa ngozi iliyoungua na jua

Maji ya viazi yatasaidia ngozi yako

Unahitaji

 • Vijiko viwili vya juisi/maji ya viazi
 • Kijiko kimoja cha asali

Cha kufanya

Changanya hivi vyote vinavyohitajika pamoja na upake kwenye uso.

Acha kama dakika 15 kisha osha.

Kausha vizuri na paka losheni au mafuta unayopenda.

 

Kuondoa mikunjo

Viazi huondoa na kupunguza mikunjo kwenye uso.

Unahitaji

 • Kiazi kimoja kilichopondwa
 • Maziwa vijiko viwili.
 • Glycerine kiasi

Cha kufanya

Katika bakuli, tia kiazi kilichopondwa na maziwa, changanya vizuri.

Ongeza gycrerine na changanya.

Paka mchanganyiko kwenye uso wako na uache kama dakika 15.

Osha kwa maji fufutende kisha ufute uso kwa taulo safi.