Makala

ULIMBWENDE: Matunda ni siri ya urembo

April 9th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

BAADHI ya watu wamekuwa wanachukulia kirahisi ulaji wa matunda, bila kujua kwamba matunda ni muhimu kwa afya zetu kwani yanatukinga dhidi ya magonjwa mbalimbali na pia husaidia katika kuboresha mwonekano mzuri wa ngozi ya miili yetu. 

Ujumbe hapa ni kwamba una kila sababu ya kuweka zingatio kwenye ulaji wa matunda kwani ni muhimu sana kwa afya pamoja na kwamba huchangia kuongeza vitamini mwilini.

Parachichi 

Tunda hili limekuwa maarufu sana kwa kutumiwa kutengeneza juisi, lakini huenda watu wakawa hawalipendi kwa sababu ya kutokuwa na sukari katika ladha yake.

Tunda hili lina vitamini kadhaa na pia huongeza mafuta mwilini kwa wale walitumialo mara kwa mara.

Unashauriwa kula au kunywa juisi ya parachichi wakati wowote endapo huna matatizo yoyote yanayohusiana na kuzidi kwa mafuta mwilini.

Tufaha

Hili ni tunda maarufu sana duniani. Tunda hili pamoja na kupewa umaarufu mkubwa kwa sababu ya kusheheni vitamini na madini, pia lina kazi kubwa sana katika kuipa ngozi muonekano mzuri.

Tunda hili husaidia kuboresha mzunguko wa damu mwilini pamoja na kuhifadhi ngozi isipoteze uhalisi wake.

Ndizi 

Hili pia ni tunda lijulikanalo na watu wengi wanaojali ulaji wa matunda, kwani nitamu na lenye ladha nzuri.

Tunda hili husaidia kulainisha ngozi ya uso iliyokauka, kwa mfano utakuta kuna baadhi ya mafuta au losheni zimechorwa ndizi.

Kula ndizi ili urekebishe ngozi ya uso wako pamoja na kuupa uwezo mzuri wa  kumeng’enya chakula.

Papai 

Ni tunda zuri hasa kama matarajio ni kuwa na ngozi yenye mafuta ya kutosha.

Papai husaidia kurudisha au kuziba sehemu zilizoumia na kunyofoka katika ngozi yako.

Papai pia hunga’arisha rangi ya ngozi yako. Yote haya ni kwa sababu ya enzyme inayotokana na papai ambayo huitwa papain.

Ikiwa unataka kutumia papai katika wajihi wako, basi chukua asali uchanganye na papai lililoiva kisha paka usoni na baada ya dakika 10, safisha.

Chungwa 

Chungwa ni tunda maarufu sana linalosaidia kurudisha ngozi iliyodhoofika ikawa nzuri kabisa na kuupa uhalisia wa ngozi yako. Jinsi ya kutumia ni rahisi sana. Chukua juisi ya chungwa kisha paka usoni na uacha kwa dakika 10 kabla ya kuosha.