Makala

ULIMBWENDE NA AFYA: Manufaa ya limau

April 11th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

LIMAU ni tunda ambalo ndani yake hupatikana vitamini C.

Kiwango cha juisi ya limau moja kinaweza kutosha kwa mahitaji ya vitamini C katika mwili wako kwa siku nzima.

Kuwepo kiwango kikubwa cha vitamini B kunamaanisha inasaidia kuzuia matatizo ya moyo na mishipa ya damu, pamoja na kusaidia kutuliza kiwango cha sukari mwilini na pia husaidia utulivu kiakili.

Malimau huwa na madini kama posferi (phosphorus), chuma (iron), magnesiamu ambayo mwili huhitaji.

Malimau husaidia kujenga kinga ya miili yetu.

Mbali na faida hizi za afya, malimau pia yanaweza kutumika katika urembo.

Zifuatazo ni mbinu chache ambazo waweza kutumia katika kuimarisha urembo wako:

Kusafisha ‘makeup’ usoni 

Kamua nusu kipande cha limau, chukua kipande cha pamba au kitambaa safi cha pamba kisha chovya kwenye maji ya limau na kisha safisha tumia kusafisha uso wako. Hapo bila shaka utakuwa umesafisha na kuongeza vitamini C katika uso wako. Kuwa makini sana isije ikaingia machoni. Safisha kwa maji mengi endapo itaingia machoni.

Kutoa alama za kuungua kwa jua na mabaka meusi

Chukua kiasi kidogo cha mlozi (ground almonds), ongeza ute wa yai na nusu kijiko cha juisi ya limau kisha uchanganye. Mchanganyiko ukishakuwa tayari, paka usoni na uacha ukae kwa muda wa dakika 20 kabla ya kuosha na kuondoa kabisa.

Husaidia ngozi ambazo ni kavu (ambazo hazina mafuta) 

Changanya vijiko vitatu vya juisi ya limau, vijiko vitatu vya asali na kijiko kimoja cha kabichi (iliochemshwa na kusagwa). Paka usoni na shingoni kisha subiri kwa dakika 10, halafu osha kwa maji baridi. Hii itasaidia kulainisha ngozi yako ya usoni na kukabiliana na ukavu wa ngozi.

Husaidia ngozi zenye mafuta 

Changanya nusu kijiko cha manjano, vijiko viwili vya limau na vijiko vitatu vya papai lililosagwa. Paka kisha subiri kwa muda wa dakika 20 kabla ya kuosha. Kutokana na vilivyomo ndani ya limau, huweza kusaidia kupunguza mafuta usoni na pia kupunguza chunusi.

Kutakatisha meno na kutoa harufu mbaya ya kinywa 

Chukua nusu limau utie chumvi kidogo na baking soda kidogo sana, utumie kuyasugua meno.

Husaidia nywele kutokatika 

Kamua limau nzima na juisi unayopata uichanganye na vijiko kama vitano vya mafuta ya nazi. Paka kichwani kisha acha kwa muda wa saa moja. Sasa unaweza ukaosha. Fanya shughuli hii angalau mara moja kwa wiki.

Huzuia mmba

Changanya juisi ya limau moja na ute wa yai moja. Paka kichwani acha kwa saa moja kisha osha. Fanya hivi kwa mwezi mmoja.

Kulainisha midomo iliokauka

Changanya mafuta kijiko kimoja, juisi ya malimau na asali. Sugulia taratibu kwenye midomo.

Hung’arisha ngozi

Changanya kiwango sawa cha nyanya iliyosagwa, juisi ya malimau na maziwa. Paka kwa muda wa dakika 10-15 kisha osha. Fanya hivi mara kwa mara.

Huchunga ngozi dhidi ya mikunjo 

Changanya kijiko kimoja cha asali, kijiko kimoja cha limau na vijiko viwili vya mafuta ya mlozi (almond) au mafuta ya zaituni(olive). Paka kwenye ngozi na uacha kwa muda wa dakika 20 kabla ya kuosha. Fanya shughuli hii angalau mara moja kila siku.