ULIMBWENDE: Njia asili za kutunza ngozi

ULIMBWENDE: Njia asili za kutunza ngozi

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

UZURI wa ngozi sio rangi tu bali ni mwonekano wa ngozi yenyewe kwamba ina afya na mng’ao unaoashiria afya njema.

Unaweza kufanya ‘facial treatment’ kwa kutumia vitu vya jikoni kama kiini cha yai, machicha ya nazi, tango na limaU. Waweza kufanya hivi mara moja kwa wiki au kila baada ya wiki mbili. Unaweza kufanya hata mara moja kwa mwezi ukipata nafasi lakini bado matokeo mazuri utayashuhudia.

Jinsi ya kufanya

Andaa maji safi yenye joto kiasi yasiyochoma ngozi yako. Osha uso wako kwa hayo maji safi.

Kama una ngozi kavu au ya kati, chukua kipande cha tango kidogo na upake yale maji yake usoni. Kwa wenye ngozi ya mafuta, wanaweza kutumia kipande cha limau kwa kupaka maji yake. Chukua pamba au kitambaa laini na futa maji ya matunda usoni kwa mtindo wa kusafisha taratibu usoni.

Chukua machicha ya nazi na anza kusugua uso na shingoni taratibu mpaka uridhike uso wote umepitiwa na machicha yako hasa unapoona unang’aa kwa mafuta kidogo yaliyotoka kwenye nazi. Kisha pukuta yale machicha ubaki na uso unaong’aa bila vitu vyeupe, yaani machicha.

Chukua kiini cha yai la kienyeji, au la kisasa lenye kiini cha njano. Ili kiini kisijichanganye na ute wakati wa kupasua, ligonge yai upande mmoja na sio katikati na limimine katika chombo mithili ya sahani ambayo unaona kiini katikati kisha unakichota na kuweka kando.

Paka ule uji mzito wa njano wa kiini kwenye uso mzima bila kusahau shingoni na nyuma ya masikio na ngozi ya masikio.

Baada ya kupaka kiini cha yai, unaweza kuendelea na shughuli zako huku likiendelea kukauka. Linapokauka ngozi yako inakuwa kama inajivutavuta.

Baada ya kule kuvuta kuisha inamaanisha yai limekauka kabisa. Osha uso wako kwa maji safi. Maji yawe ya baridi sasa.

Kuosha uso kwa maji yenye joto kunafungua matundu ya ngozi.

Tango au limau hutumika kama kisafishaji. Unapokuja kujifuta taratibu unaondoa uchafu katika ngozi yako.

Machicha ya nazi yanatumika kama skrabu, yanaondoa seli zilizokufa, kuifanya ngozi kuwa laini na kuipa mng’ao.

Kiini cha yai hapa kinatumika kama maski na pia huwa na vitamini E.

Faida za kufanya hivyo

  • husaidia kutibu na kuikinga ngozi dhidi ya chunusi,
  • huipa ngozi mng’ao bila kutumia kemikali za sumu,
  • husaidia kupunguza mikunjo katika ngozi yako
  • inachukua gharama ndogo kuifanya.
  • Tags

You can share this post!

MAPISHI: Nyama ya kuku yenye ukavu na utamu wa kipekee

Wakazi wa Ol Moran wasita kurejea kwao