Makala

ULIMBWENDE: Tumia mbinu hii ya vitunguu maji kutunza nywele

August 1st, 2018 2 min read

Na MARGARET MAINA

MTU na hasa mwanamke anayetambua umuhimu wa mwonekano mzuri hutamani kuwa na nywele nzuri za kutosha na zenye afya yake ya asili. Tatizo la kupotea kwa nywele au upara (wengine hupenda hali hii) limekuwepo tangu awali. Kipara kinaweza kuja kwa sababu za kimaumbile za kawaida.

Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha kupotea kwa nywele kama vile:

 • Sababu za kimazingira
 • Kuzeeka
 • Msongo wa mawazo (stress)
 • Kuvuta sigara kupita kiasi
 • Lishe duni
 • Homoni kutokuwa sawa
 • Kurithi vinasaba
 • Maambukizi kwenye ngozi ya kichwa
 • Matumizi yasiyo sahihi ya vipodozi vya nywele
 • Baadhi ya dawa za hospitali
 • Matatizo katika kinga ya mwili
 • Upungufu wa madini chuma, na
 • Magonjwa mengine sugu

Kitunguu maji kina kazi nyingi katika mwili wa binadamu kwani hutibu magonjwa mengi kama kikohozi, vidonda vya tumbo na mifupa, ngozi, koo, figo, na pia kina virutubisho vingi vya vitamini C.

Kitunguu hiki huwa na salfa (sulphur) ambayo husaidia kutengeneza tishu za ‘collagen’ katika mwili ambapo huipa nywele na ngozi nuru ya aina yake.

Hivyo naweza kusema kuwa juisi ya kitunguu maji husaidia kukuza nywele na kwa wale wenye nywele za kukatika, kupaka kitunguu maji mara kwa mara kunaweza kusaidia kupambana na tatizo hilo.

Jinsi ya kuandaa

 • Chukua kitunguu kimoja au viwili kutegemea na na ukubwa wa kitunguu chenyewe
 • Osha vizuri kitunguu au vitunguu na kisha ukimenye au uvimenye
 • Kata kitunguu au vitunguu vipande vidogo vidogo ili iwe rahisi kusaga au kutwanga
 • Saga kwenye blenda au uvitwange kwenye kinu.
 • Visage au vitwange mpaka vilainike kabisa ili uweze kutoa maji kwa urahisi.
 • Vichuje vizuri ili upate majimaji. Hakikisha kwamba huongezi maji kwa hivi vitunguu.

Jinsi ya kupaka

Nywele sio lazima ziwe safi maana unapaswa kuziosha baada ya kupaka maji ya vitunguu.

 • Chukua pamba ambayo utatumia kupaka hayo maji ya vitunguu kwenye nywele zako. Paka zile sehemu ambazo nywele zimekatika. Unaweza pia paka kichwa kizima.
 • Baada ya kupaka unapaswa kuvaa kofia ya plastiki na kitambaa kichwani ili uweze kupata joto.
 • Ukae hivyo kwa muda wa saa 4 – 5
 • Baada ya hapo unaweza kuosha na kukausha nywele zako.

Hitimisho

Ni vyema kufanya shughuli hii ya kupaka vitunguu angalau mara mbili kwa mwezi.

Ikiwa harufu ya kitunguu ni kali, unaweza kuongezea asali kidogo kwenye maji ya vitunguu.

Kwa matokeo mazuri ya kukuza na kutunza nywele zako, tumia vitunguu vidogo kufanya jinsi nilivyoeleza hapo juu.