Makala

ULIMBWENDE: Viini vya mipasuko ya visigino na jinsi ya kuzuia na kutibu

July 31st, 2018 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MTU kuwa na miguu au visigino vilivyopasuka ni dalili tosha kuwa katika mwili kuna upungufu wa virutubisho kadhaa, vitamini au madini.

Hata hivyo, wengi wetu tumekuwa na mitazamo kwamba visigino kupasuka ni ishara tosha kwamba mtu ameonyesha kutojali usafi wa miguu yake.

Kwa kawaida, ngozi zetu huwa zina unyevu ambao huiwezesha ngozi ivutike au kutanuka pamoja na kusinyaa bila ya kutokea madhara yoyote kama vile kuchanika.

Pamoja na ngozi kugawanyika katika sehemu tatu; yaani sehemu ya nje ‘Epidermis’, sehemu ya kati ‘Dermis’ na sehemu ya ndani ‘Endodermis’, ni sehemu ya nje, ambayo ipo karibu na unaweza kuigusa au inaweza kuathirika na ukaiona kirahisi; na hii ni kwa sababu inagusana moja kwa moja na mazingira yetu.

Mitembo huanza kutokea katika sehemu hii ya ngozi, Epidermis.

Miongoni mwa sababu zinazoweza kumfanya mtu apasuke visigino ni pamoja na:

a) Ngozi kuwa kavu sana

Hii ni sehemu ya nje ya ngozi ambayo inawezekana mtu kwa asili yake akawa na ngozi kavu na hivyo kuifanya ishindwe kustahimili kutanuka au kusinyaa na hivyo kusababisha ipasuke.

Kuiacha miguu katika maji kwa muda mrefu na baadaye kutoipaka mafuta ya kulainisha ngozi husababisha ile asili ya ngozi pamoja na mafuta katika ngozi yapotee na kuiacha ngozi ikiwa kavu sana.

b) Kuwa na uzito mkubwa

Hali hii husababisha presha kubwa iwe katika miguu unapokanyaga chini na endapo ngozi yako haitakuwa na uimara wa kutosha itasababisha visigino vipasuke.

Upungufu wa virutubisho mwilini; hasa madini ya Zinc, vitamini E pamoja na mafuta, na Omega 3. Hii husababisha ngozi kupoteza uimara wake na kuifanya ipasuke.

c) Kuvaa viatu ambavyo nyuma vipo wazi

Hulazimisha mguu au upande wa kisigino katika mguu utanuke zaidi na hivyo kuuweka mguu hatarini kupasuka.

d) Magonjwa

Baadhi ya maradhi kama vile Kisukari na magonjwa ya homoni (thyroid diseases) yana athari hasi kwa afya ya ngozi.

e) Umri mkubwa

Kwa kawaida mtu anapokuwa na umri mkubwa sana, hata utendaji kazi wa mifumo mbalimbali katika mwili wake hupungua kiufanisi; hivyo hata kinga ya mwili pamoja na afya ya ngozi pia hupungua.

Mtu kutozingatia usafi wa miguu yake kwa kiwango kinachostahili pia husababisha mipasuko kwenye visigino.

Moja ya madhara yanayoweza kutokea kwa mtu kupasuka visigino ni kupata maambukizi ya magonjwa.

Hii ni endapo miguu itachanika kiwango cha kufikia dermis, kiasi cha kusababisha damu ianze kutoka na kuchangia maumivu makali.

Mtu anaweza kupata maambukizi ya magonjwa kupitia mipasuko hiyo.

Kuzuia au kutibu tatizo la kupasuka visigino

Unafaa:

  • Kuzingatia ipasavyo usafi wa miguu na mwili kwa ujumla.
  • Kuepuka kutembea katika sehemu zisizo sawa bila kuvaa viatu, hii itaepusha miguu kuchanika.
  • Kwa miguu iliyopasuka tayari, ifanyie usafi miguu yako na kisha tumia mafuta ya mzaituni kupaka sehemu zilizo na mipasuko.
  • Vaa soksi na viatu vya kufunika ili miguu iendelee kuwa na unyevu. Usiku pia fanya hivyo kwa kuhakikisha ukilala miguu imevalishwa soksi baada ya kwamba umeipaka mafuta.
  • Hakikisha unakula vyakula venye madini ya calcium, zinc na iron. (Maziwa, mboga za majani, mafuta ya mimea, nyama, maharage pamoja na samaki)
  • Epuka kusimama kwa muda mrefu pamoja na kutoiweka miguu katika maji kwa kipindi kirefu.
  • Kama unafua jitahidi kuilinda miguu yako isiwe kwenye sabuni kwani aina nyingi za sabuni ya kufulia huvunjavunja mafuta yaliyo katika ngozi na kuiacha ikiwa kavu sana.
  • Jitahidi angalau mara moja kwa wiki kuiweka miguu yako katika maji moto. Hii husaidia kuongeza mzunguko wa damu katika miguu na hivyo kuendelea kuimarisha afya ya ngozi yako.