Makala

ULIMBWENDE: Vya kuepuka unapokuwa na ngozi kavu

August 28th, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

NGOZI ni kiungo muhimu sana katika mwili wa binadamu.

Inafanya kazi mbalimbali kama vile kuulinda mwili, kusaidia kutoa taka mwilini, kusaidia kuratibu na kudhibiti kiwango cha joto, maji na chumvi ya mwili pamoja na kuhisi kama vile joto, baridi, miguso, mkandamizo na kadhalika kutoka nje ya mwili.

Mbali na hayo, ngozi ni sehemu muhimu sana katika muonekano na uzuri wa mwili.

Ngozi ikiwa nzuri na mwili huwa vizuri, ngozi ikiwa vibaya na mwili pia huweza kuwa vibaya.

Ngozi kavu inaweza kukufanya ukose raha kutokana na kuwasha mara kwa mara, lakini pia kukauka kunaweza kusababisha mikunjo ya ngozi na hata kusababisha vidonda katika ngozi.

Ngozi kavu husababishwa na baridi lakini pia unaweza ukawa umezaliwa nayo tu ukawa upo hivyo. Ikiwa una ngozi ya aina hii, basi haya ni mambo na vitu unavyopaswa kuepuka kufanya.

Kuoga maji ya moto kwa muda mrefu

Kuepuka kuoga maji moto mara kwa mara kunaweza kufanya yale mafuta ya asili yanayoupa mwili mng’ao kukauka. Ili kuepuka tatizo hili, ni vyema ukatumia maji ya ufufutende au baridi katika kuoga au kunawa.

Kutumia vipodozi vyenye kiwango kikubwa cha alkoholi

Kiwango kikubwa cha alkoholi husababisha ngozi kuzidi kuwa kavu. Wakati wa kwenda kununua vipodozi vyako hakikisha unasoma maelezo na kujua kiasi cha alkoholi kilichomo. Kama ni kingi, achana nacho na uchukue kipodozi chenye kiasi kidogo.

Kuosha ngozi kwa kutumia sabuni mara kwa mara na kuisugua kwa nguvu

Kuosha ngozi mara nyingi sana na sabuni ni njia ya mojawapo ya kupata ngozi kavu. Ngozi kavu huathirika zaidi na maambukizi ya bakteria kwa sababu kuosha mara nyingi huondosha safu za kinga ambazo ni muhimu kwa ngozi.