Michezo

Ulinzi kuwakosa nyota wawili katika gozi na Sofapaka

September 12th, 2019 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

ULINZI Stars watakosa huduma za beki Omar Mbongi na kiungo Brian Birgen watakaposhuka dimbani kuchuana na Sofapaka katika kivumbi cha Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kitakachorejelewa wikendi hii.

Wawili hawa walikosa mchuano wa ufunguzi wa msimu huu uliowashuhudia Ulinzi Stars ambao ni mabingwa mara nne wa taji la KPL, wakiwakomoa limbukeni Kisumu All Stars 2-0.

Kwa mujibu wa John Imboywa ambaye ni tabibu wa Ulinzi Stars, Mbongi anaugua malaria huku Birgen akiuguza jeraha la mguu alilolipata wakati akiwawajibikia waajiri wake katika mechi za majuzi za Majeshi ya Afrika Mashariki.

“Huenda Birgen akasalia mkekani kwa kipindi cha hadi mwezi mmoja kutokana na jeraha. Kwa upande wake, Mbongi anatarajiwa kurejelea mazoezi hii leo, na huenda asiwe katika hali nzuri ya kuwajibishwa wikendi,” akasema Imboywa.

Kukosekana kwa Birgen kunawaweka Ulinzi Stars katika ulazima wa kutegemea huduma za chipukizi wa Harambee Stars, Ibrahim Shambi aliyekosa mechi dhidi ya Kisumu All Stars.

Michuano yote miwili iliyowakutanisha Ulinzi na Sofapaka msimu jana ilikamilika kwa sare ya 2-2.

Sofapaka watapania kujinyanyua baada ya mchuano wao wa ufunguzi wa kampeni za msimu huu kukamilika kwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Posta Rangers.

Kwingineko, AFC Leopards watakuwa na kapteni mpya watakapovaana na Kariobangi Sharks.

Jeraha linalouguzwa na Robinson Kamura kunampa kiungo Whyvonne Isuza fursa ya kuvalia utepe wa unahodha.