Habari Mseto

Ulinzi mkali kamanda akizikwa, mke asusia

November 24th, 2019 1 min read

Na STEVE NJUGUNA

Kamanda wa zamani wa kikosi cha jeshi la angani Kenya, Meja Jenerali Duncan Kireri Wachira, hatimaye alizikwa Ijumaa nyumbani kwake Runda, Nyandarua chini ya ulinzi mkali huku mkewe wa kwanza na watoto wake wakisusia mazishi.

Meja Jenerali Wachira ambaye alikuwa kamanda wa kikosi hicho kati ya 1989 na 1994, alifariki kutokana na ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu katika Hospitali ya Nairobi, maradhi ambayo aliugua kwa zaidi ya miaka mitano.

Kifo chake kilifufua mzozo wa muda mrefu kuhusu mali yake kati ya Bi Margaret Wakonyo, yaya aliyemuoa miaka 19 iliyopita kama mke wake wa pili na wanawe wawili kutoka ndoa ya kwanza.

Baada ya kifo chake mnamo Oktoba 22, mipango ya kumzika marehemu ilisitishwa baada ya Bi Wakonyo na watoto wake wa kambo kuhusika kwenye ugomvi juu ya mali ya Meja Wachira, mali ambayo ni pamoja na shamba la mifugo huko Limuru, kaunti ya Kiambu, nyumba tatu za makazi jijini Nairobi na jengo la kibiashara lililoko Ongata Rongai viungani vya jiji la Nairobi.

Meja Jenerali Wachira alimuoa Bi Wakonyo ambaye aliwahi kuhudumu kama yaya wake miaka mitatu baada ya kumpa talaka mke wake wa kwanza, Ann Wanjiru, mwalimu wa zamani wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Pangani.

Katika ndoa ya kwanza, walikuwa wamebarikiwa na watoto wanne, Marehemu Allan Wachira, Michael Wanjohi, Edward Thiong’o na Sylvia Muthoni.

Kabla ya kifo chake, watoto wake wawili (Wanjohi na Thiong’o) walikuwa wamemshutumu baba yao kwa madai ya kuhamisha umiliki wa mali yake kwa mke wake wa pili jambo ambalo liliwafanya kumshtaki katika Mahakama Kuu.

Lakini mahakama ilimpa Bi Wakonyo agizo la kujumuishwa kama mmoja wa wasimamizi wa mali ya Meja Jenerali Wachira na pia kuwa mwangalizi wa Bw Wachira ambaye wakati huo alikuwa akiugua.