Michezo

Ulinzi, Nairobi Water na NCPB kuwakilisha Kenya katika handiboli Cameroon

April 26th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KENYA itashiriki kipute cha kuwania ubingwa wa Afrika katika fainali za handiboli kwa klabu za wanawake zitakazoandaliwa jijini Yaounde, Cameroon.

Haya ni kwa mujibu wa mkurugenzi wa kiufundi wa Shirikisho la Handiboli la Kenya (KHF), Charles Omondi ambaye amefichua kwmaba Kenya itawakilishwa na vikosi vitatu.

Mbali na Ulinzi, klabu nyinginezo zitakazopeperusha bendera ya Kenya nchini Cameroon mashindano hayo yatakapoandaliwa mnamo Agosti 2020, ni National Cereals and Produce Board na Nairobi Water.

“Tumepokea kalenda mpya kuhusu jinsi kivumbi cha bara la Afrika kitakavyoendeshwa na kwa sasa tunajitahidi kupata uakilishi katika vitengo vyote vinne za mashindano hayo,” akasema Omondi huku akiahidi kufichua ratiba itakayoongoza shughuli zao za mazoezi licha ya janga la corona ambalo kwa sasa limesitisha michezo yote duniani.

“Tunashauriana na wadau wote na tutatoa mwongozo kuhusu namna klabu husika zitakavyorejea kambini kwa minajili ya kujiandaa kwa mapambano ya bara,” akaongeza.

Licha ya kufichua viwanja vitakavyotumiwa kuandalia fainali hizo, Shirikisho la Handiboli la Afrika (CAHB) bado halijatoa tarehe mahsusi ya kufanyika kwa michezo hiyo iliyoahirishwa kutoka Aprili hadi Agosti 2020.

“Nina hakika kwamba vikosi vyetu vya wanawake vina uwezo wa kunyakua ubingwa wa Afrika na kufuzu kwa kipute cha kuwania Kombe la Dunia. Hata hivyo, haya ni mafanikio yatakayowezekana iwapo tu tutaanza kujiandaa mapema,” akasisitiza Omondi.

Kwa mujibu wa CAHB, mapambano yote mengine ya handiboli kwa upande wa wanaume (watu wazima) na vikosi vya chipukizi (wasichana) wasiozidi umri wa miaka 17 yataandaliwa jijini Cairo, Misri. Ni mechi za wanawake (watu wazima) tu ndizo zitakazofanyika Yaounde.

“Tutatoa tarehe kamili za kufanyika kwa mashindano haya wakati wowote mwezi huu. Japo tunatazamia kufanikisha mapambano yenyewe Agosti, tutawasiliana na washikadau katika mataifa husika kadri hali itakavyokuwa kuhusiana na janga la sasa la corona,” ikasema sehemu ya taarifa ya CAHB.

Mashindano ya handiboli kwa wavulana wasiozidi umri wa miaka 17 yataandaliwa jijini Casablanca, Morocco.