Ulinzi Starlets pazuri kumaliza katika nafasi ya pili KWPL

Ulinzi Starlets pazuri kumaliza katika nafasi ya pili KWPL

Na JOHN KIMWERE

MAAFANDE wa Ulinzi Starlets wamejiongezea matumaini ya kumaliza katika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Wanawake (KWPL), walipokung’uta Kisumu All Starlets kwa mabao 4-0 kwenye mechi iliyopigiwa uwanjani Ruaraka, Nairobi.

”Ninashukuru wachezaji wangu kwa kujituma vilivyo na kutia kapuni alama tatu muhimu,” kocha wa Ulinzi, Joseph Mwanza alisema na kuongeza kuwa ana imani wakiendelea hivyo watatimiza azma yao.

Nao waliokuwa mabingwa watetezi, Thika Queens waliteleza na kutoka nguvu sawa mabao 2-2 na Trans Nzoia Falcons, huku Vihiga Queens ambayo tayari imetwaa taji hilo ikizoa mabao 5-0 dhidi ya Kangemi Starlets.

Sheryl Angachi alicheka na wavu mara mbili nao Mercy Airo na Jentrix Kuyudi kila mmoja alifunga bao moja na kusaidia Ulinzi kubeba alama tatu muhimu na kuendelea kukamata nafasi ya pili katika jedwali.

Gaspo Women ilisajili ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Bunyore Starlets na kurukia tatu bora kwa alama 36, moja mbele ya Thika Queens.

Vihiga ya kocha, Boniface Nyamunyamu ilipata ufanisi kupitia Topister Situma mabao mawili, nao Maurine Achieng Ater, Faith Ongachi na Eve Chemutai Selim kila mmoja alitikisa wavu mara moja.

Nayo Trans Nzoia Falcons ilitangulia kufunga mabao hayo kupitia Noel Aruko kabla ya Rebecca Akinyi na Wendy Achieng kusawazishia Thika Queens kwa kufunga goli moja kila mmoja.

Gaspo Women ya kocha, Domitila Wangui ilibeba ufanisi huo kupitia juhudi za Adrine Birungi aliyetikisa wavu mara mbili.

Nao vipusa wa Kayole Starlets waliendelea kuona giza walipokubali kichapo cha goli 1-0 mbele ya Nakuru City Queens.

Katika msimamo wa ngarambe hiyo, Vihiga Queens inaongoza kwa alama 53 ikiizidi Ulinzi Starlets kwa alama 15.

Wachezaji wa Ulinzi Starlets wakishiriki mazoezi kabla ya kushuka dimbani kucheza mechi ya Ligi Kuu ya Kenya (KWPL). PICHA | JOHN KIMWERE
  • Tags

You can share this post!

Kocha Ten Hag ateua wakufunzi watakaomsaidia kunoa kikosi...

Barbara Waweru ‘Mama Nyambu’ ni mwigizaji...

T L