Michezo

Ulinzi Warriors wasajili wanavikapu wawili

September 14th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA wa kitaifa wa mchezo wa vikapu, Ulinzi Warriors, wamejinasia huduma za wachezaji wawili kwa minajili ya kampeni za msimu ujao katika Ligi Kuu ya Shirikisho la Vikapu la Kenya (KBF).

Meneja wa timu hiyo, Stephen Bartilol, amethibitisha kwamba Brans Nzioka na Gideon Ndambuki ndio wanavikapu wapya ambao wamesajiliwa na Warriors kutoka kambini mwa Laiser Hill Academy.

“Tumesajili wachezaji wawili wa haiba kubwa kutoka Laiser Hill. Wamekuwa wakishiriki mazoezi ya pamoja na wanavikapu wetu na wakaridhisha vinara wa benchi ya kiufundi,” akasema Bartilol kwa kusisitiza kwamba ujio wao utaimarisha safu ya na mbele kiasi cha kuwaweka Warriors pazuri zaidi kuhifadhi ufalme wao msimu huu.

“Wanaelewa vyema malengo yetu na ni matumaini ya kila mmoja kwamba watatulia kambini haraka iwezekanavyo na kuoanisha mtindo wa mchezo waliozoea hapo awali na huu wetu wa sasa,” akaongeza.

Mbali na maazimio ya kuhifadhi ubingwa wao wa kitaifa wa KBF, Warriors wanapania pia kutamba kwenye Michezo ya Majeshi barani Afrika mwakani na katika Ligi ya Vikapu barani Afrika (BAL) itakayonogeshwa kuanzia Januari 2021.

“Warriors ndio wawakilishi wa pekee wa Kenya kwenye kipute cha BAL na Michezo ya Majeshi. Matarajio ni ya juu zaidi, nasi tumepania kutia fora na kuridhisha zaidi wadhamini na mashabiki wetu,” akasema Bartilol.

“Zaidi ya kuelekezwa mitandaoni, wachezaji wamekuwa wakishiriki mazoezi kivyao kwa muda mrefu na sasa wamerejea kambini kwa mazoezi ya pamoja yanayoendeshwa katika makundi ya watu wachache,” akafichua.

Kenya iliambulia nafasi ya tatu kwenye Michezo ya Majeshi iliyoandaliwa ugani MISC Kasarani mwaka jana.

Bartilol ameshikilia kwamba kubwa zaidi katika maazimio yao ni kusuka kikosi kitakachorejesha ubingwa wa taji hilo la Majeshi humu nchini mwaka ujao.

Mnamo 2019, Warriors waliwakung’uta Thunder katika fainali na kutwaa taji la Ligi Kuu ya Vikapu (KBF) kwa jumla ya alama 31-27 chini ya kocha William Balozi.

“Tumetambua idara zinazohitaji kufanyiwa mabadiliko muhimu ili kuipa timu mseto wa wanavikapu chipukizi watakaoleta nguvu mpya na kushirikiana vilivyo na wachezaji wazoefu,” akasema Balozi aliyetegemea sana wanavikapu Eric Mutoro, James Mwangi na Victor Bosire katika kampeni za muhula uliopita.