Michezo

Ulinzi yapanga kuinyeshea Vihiga mvua ya magoli

July 19th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

KLABU ya Ulinzi Stars inalenga kuwalisha kichapo mahasimu wao Vihiga United, timu hizo zitakapokutana Jumapili 22, 2018 kwenye mechi ya kombe la ngao la FKF raundi ya 16. 

Wanajeshi hao waliwashinda Vihiga United 2-0 katika mechi ya KPL iliyosakatwa katika uwanja wa Mumias Complex Jumapili 15,2018 na mechi ya Jumapili itakayogaragazwa ndani ya uwanja uo huo inatarajiwa kusimimua kwa kuwa Vihiga watakuwa wakilenga kulipiza kisasi.

Hata hivyo kocha wa Ulinzi Stars Danstone Nyaudo amewataka vijana wake kutowapuuza wapinzani na badala yake wabuni mbinu zitakazowasaidia kuibuka na ushindi.

‘’ Si rahisi kushinda mara mbili kwa mpigo dhidi ya timu moja kwa sababu wanaelewa mbinu tulizotumia kwenye mechi ya awali. Hata hivyo tutabuni mbinu nyingine ili kuwakomoa,’’ akasema Nyaudo.

Timu hizo zimetwaa ushindi mara moja kila moja katika mechi mbili za KPL zilizowakutanisha awali na atakayeshinda atafuzu kuingia hatua ya robo fainali ya kombe hilo.

Ulinzi wanalenga kujiimarisha baada ya kusajili matokeo yasiyoridhisha wakiwa wameshinda mechi tatu kati ya 12 walizoshiriki katika michuano mbalimbali.

Bingwa mtetezi wa kombe hilo ambalo awali lilikuwa likiitwa ngao ya GOtv ni AFC Leopards.