Michezo

Ulinzi yatoka sare na Uganda

August 16th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya kumiminia Burundi mabao 4-0 katika mechi yake ya ufunguzi ya michezo ya wanajeshi kutoka Muungano wa Afrika Mashariki, wawakilishi wa Kenya, Ulinzi Stars, waliishiwa na ‘risasi’ wakiumiza nyasi bure dhidi ya Uganda, Ijumaa.

Mabingwa watetezi Ulinzi walitikisa nyavu za Burundi mara tatu kupitia kwa Oscar Wamalwa naye mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Kenya wa msimu 2018-2019 Enosh Ochieng’ akachangia bao moja uwanjani Kasarani katika mechi ya kufungua mashindano haya ya kila mwaka mnamo Agosti 13.

Hata hivyo, mabao ya Ulinzi yalikauka iliporejea uwanjani kuzichapa dhidi ya Waganda, ambao pia walianza mashindano kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Rwanda mnamo Agosti 14.

Timu za Kenya na Uganda zilishambulia lango la mwenzake, lakini baada ya dakika 90 hakuna aliyefanikiwa kupata bao.

Tanzania

Ulinzi itakuwa na siku mbili bila mechi kabla ya kusakata mechi yake ya tatu ambayo itakuwa dhidi ya Tanzania mnamo Agosti 19.

Tanzania ilianza kampeni yake kwa kuongezea Burundi masaibu baada ya kunyuka 7-3 Agosti 15 uwanjani humo. Rwanda na Burundi watakabana koo hapo Agosti 17.