Michezo

Ulinzi Youth na Falling Waters majogoo wa Mlima Kenya

January 20th, 2020 3 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Ulinzi Youth na Falling Waters zilitawazwa mafahali na malkia wa Chapa Dimba na Safaricom Season Three katika Mkoa wa Kati baada ya kufanya kweli katika fainali zilizopigiwa mjini Nanyuki.

Ulinzi Youth chini ya kocha, Vincent Otieno na Falling Waters ziliibuka mabingwa baada ya kila moja kuvuna mabao 3-1 dhidi ya JYSA FC na Limuru Starlets mtawalia.

Wasichana wa Falling Waters awali wakifahamika kama Barcelona Ladies walihifadhi taji hilo na kunasa tiketi ya kuwakilisha eneo hilo kwa mara ya pili mfululizo katika fainali za kitaifa zitakaopigiwa mjini Mombasa Mwezi Juni mwaka huu.

Wasichana wa Falling Waters wakituzwa baada ya kutwaa tajila Chapa Dimba na Safaricom Season Three /20192020 katika fainali za Mkoa wa Kati.

Licha ya wavulana wa JYSA kutangulia kufunga kupitia Clinton Sheitara dakika ya tisa waliangukia pua baada ya wapinzani wao kuzinduka na kuwazidi maarifa.

Brian Kafero alisawazishia Ulinzi dakika 20 baadaye kabla ya Emmanuel Lenkai na Kelvin Akmat kufunga mara moja kila mmoja dakika ya 34 na 72 mtawalia.

”Kama ilivyo ada yangu huchukua dakika za kwanza kusoma jinsi wapinzani wetu wanavyocheza kisha kukipanga kikosi changu propa,” alisema kocha huyo wa Ulinzi Youth na kuongeza kuwa hakuna kulaza damu watazamia mazoezi yao ili kujiweka vizuri kukabili wapinzani wao katika fainali za kitaifa.

Wavulana wa Ulinzi Youth wakituzwa baada ya kutwaa taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Three /20192020 katika fainali za Mkoa wa Kati.

Matumaini ya Limuru Starlets ya kocha, James Kairu kusonga mbele yaligonga ukuta ilipokubali kulala mbele ya wapinzani wao.

Chipukizi hao waliteremsha soka safi na kuonyesha wangali ng’ang’ari kwenye kampeni za ngarambe ya mwaka huu kama msimu uliyopita.

Falling Waters ililazimishwa kusubiri kwa dakika tisa kabla ya kupata bao la kwanza lililopachikwa kimiani na Miriam Lutomia.

Jane Njeri wa Falling Waters akituzwa baada ya kuibuka mfungaji bora kwa wasichana katika fainali za Chapa Dimba na Safaricom Season Three /20192020 katika Mkoa wa Kati.

Mchezo huo uliendelea kunoga huku Falling Waters ikionekana kulemea wapinzani wao waliokuwa wanajituma kisabuni dimbani.

Jane Njeri aliyeibuka mfungaji bora katika kipute hicho alihakikishia wasichana hao ubingwa huo alipotikisa wavu mara mbili dakika ya 65 na 74. Joy Kanja aliibuka shujaa alipotia Limuru Starlets bao la kufuta machozi dakika ya 82.

”Hakuna kupumua tutazidi kupigania taji hilo hata baada ya kulikosa kwa mara ya pili mfululizo,” alisema kocha huyo wa Limuru Starlets na kuongeza kuwa licha ya kushindwa wachezaji wake walionekana kuimarika zaidi kinyume na walivyokuwa muhula uliyopita.

Brian Katero wa Ulinzi Youth akituzwa baada ya kuibuka mfungaji bora kwa wavulana

Kando na tiketi ya kushiriki fainali mabingwa hao kila moja ilituzwa kitita cha Sh200,000 na kampuni ya Safaricom ambayo hufadhili mashindano hayo. Nazo JYSA na Limuru Starlets kila moja ilitia kibindoni zawadi ya Sh100,0000.

Mabingwa wa kitaifa kama kawaida watapokea kitita cha Sh 1 milioni. Mashindano ya kipute hicho makala yaliyopita yamefanikiwa kukuza wachezaji wengi ambao wamebahatika kujiunga na klabu tofauti nchini zinazoshiriki ngarambe ya Betika Supa Ligi (BNSL) bila kusahau Ligi Kuu ya KPL.

Hannah Namuya (kulia) wa Falling Waters akishindana na Damaris Akinyi wa Limuru Starlets

Nusu fainali

JYSA ya Juja ilitoka chini baada ya kupigwa bao 1-0 na kusajili ufanisi wa mabao 2-1 dhidi ya Irigiro FC ya Maragua kwenye nusu fainali.

Nao wavulana wa Kimatugu kutoka Kirinyaga walirandwa bao 1-0 na Ulinzi Youth ya Nanyuki lililofumwa kimiani na Brian Kafero.

Kwenye nusu fainali za wasichana, Karima Queens ya Nyeri ilibebeshwa kapu la magoli 12-0 na Falling Waters ya Laikipia.

Jane Njeri alifungia Waters mabao manne na kujiongezea tumaini la kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa kike. Nao wachana nyavu wa Limuru Starlets walipararua Achievers ya Ruiru kwa mabao 5-1.

Winfred Mukami (kulia) wa Limuru Starlets akishindana na Jane Njeri wa Falling Waters katika fainali ya wasichana kuwania taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Three

Wapigagozi bora watuzwa

Kwa mara nyingine, Jane Njeri wa Falling Waters aliyetingia timu yake mabao mengi msimu uliyopita aliibuka mfungaji bora baada ya kucheka na wavu mara sita. Kwa wavulana tuzo hiyo ilimwendea

Brian Kafero kwa kufunga mara mbili.

Nao Elijah Mambo wa Ulinzi Youth na Eunice Alele mchezaji wa Falling Waters waliibuka wanyakaji bora kwa wavulana na wasichana mtawalia.

Dickson Elegae (kushoto) akikabiliana na mchezaji wa Ulinzi Youth, George Okwaro katika fainali ya wavulana kupigania taji la Chapa Dimba na Safaricom Season

Nayo tuzo ya mchezaji anayeimarika kwa wavulana na wasichana ilinyakuliwa nao Kelvin Akmat (Ulinzi Youth) na Miriam Lutomia (Falling Waters).

Washindi hao wamejiunga na wenzao kutoka maeneo mengine ikiwamo wavulana wa Berlin FC ya Garissa (Mkoa wa Kaskazini Mashariki) na Yanga FC kutoka Malindi Mkoa wa Mombasa.

Kwa wasichana Falling Waters walimeunga na Kwale Ladies kutoka Kwale malkia wa taji hilo katika Mkoa wa Mombasa.