Ulipaji fidia kwa wakazi wa Lamu ni kabla ya Juni

Ulipaji fidia kwa wakazi wa Lamu ni kabla ya Juni

Na ANTONY KITIMO

Wakazi wa Lamu walioathiriwa na ujenzi wa bandari sasa wanaweza kutabasamu baada ya Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA) kutangaza mipango ya kuwalipa fidia.

Aidha, KPA imeanza kuweka vifaa katika bandari hiyo ya Lamu kabla ya kufunguliwa hapo Juni.Mamia ya wakazi wa Lamu walioathiriwa na mradi wa Bandari ya Lamu na mradi wa uchukuzi hadi Sudan Kusini na Ethiopia (LAPSSET) pia wamehakikishiwa fidia yao kabla ya bandari kuanza shughuli zake.

Wiki jana, waziri wa Fedha, Bw Ukur Yatani alitembelea bandari ya Lamu kukagua mradi huo na kuwahakikishia wakazi kwamba watalipwa fidia yao inayokadiriwa kuwa Sh1.76 bilioni.

Kulingana na KPA, maandalizi ya orodha ya mwisho ya watakaolipwa fidia hiyo yameanza na mkutano wa umma utaitishwa kuanzia wiki hii kuthibitisha watakaonufaika kabla ya pesa hizo kutolewa.

“Tutalipa na tutashirikiana na wakazi wa jamii ya hapa na ulipaji wa fidia ni suala tunalolipatia nafasi ya kwanza, na utafanyika baada ya orodha ya mwisho kuwa tayari,” alisema mkuu wa masuala ya biashara Benard Osero.

Vifaa vya mabilioni ya pesa viliondoka bandari ya Mombasa kuelekea Lamu mwishoni mwa wiki huku KPA ikiwa katika harakati za mwisho za kuhakikisha bandari hiyo mpya itakuwa tayari kufunguliwa ilivyopangwa. Vifaa hivyo vinatarajiwa kuwasili Lamu leo.

Naibu afisa wa mafunzo na shughuli za vifaa katika KPA anayesimamia bandari ya Lamu, Bw Ernest Mbalanya alisema kwamba shehena ya pili ya vifaa itaondoka bandari ya Mombasa kuelekea Lamu Mei 15 kuunganishwa kabla ya bandari kufunguliwa Juni.

“Vifaa vya kwanza ni magari na matrela lakini katika awamu ya pili tutasafirisha kreni kubwa ambazo zitakuwa za mwisho kuwekwa kabla ya meli ya kwanza kutia nanga Juni,” alisema Bw Mbalanya.

Aliongeza kuwa tayari wafanyakazi wa kutosha wametumwa kuhakikisha bandari hiyo itakuwa ikihudumu kikamilifu itakapofunguliwa.Baadhi ya vifaa vinavyotarajiwa kusafirishwa ni matingatinga, matrela 14, magati ya magurudumu 14, mashua, ambulensi na gari la kuzima moto miongoni mwa vingine.

Bw Mbalanya alisema kwamba vifaa zaidi vinatarajiwa kununuliwa kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022. Kabla ya bandari kufunguliwa rasmi, KPA itawafidia wote walioathiriwa.

KPA pia imeunda kamati maalumu ya kutangaza bandari ya Lamu kwa wafanyabiashara wa Ethiopia, Somalia na Sudan Kusini kabla ya kufunguliw Juni 15.

Kamati hiyo tayari inawasiliana na wadau tofauti kuwashawishi kuanza kutumia bandari ya pili ya Kenya ambayo itashughulikia bidhaa zinazoelekea mataifa mengine miezi miwili ya kwanza baada ya kufunguliwa.

You can share this post!

Orengo apendekeza Oburu Odinga kumrithi useneta Siaya

Mahangaiko tele familia zilizofurushwa katika ardhi zao...