Makala

Umaarufu wa Ruto Mlima Kenya taabani Gachagua na Nyoro wakiraruana 

January 14th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI 

MALUMBANO kati ya Naibu wa Rais Rigathi Gachagua na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro yamechacha huku sasa Rais William Ruto akionywa vikali kwamba uchaguzi mkuu wa 2027 hautakuwa rahisi kwake.

Rais Ruto ameambiwa na washirika wa Nyoro kwamba haitakuwa mteremko kwake 2027 kama ilivyokuwa 2022 ikiwa ataandamana na Gachagua kama mgombea mwenza wake.

Eneo la Mlima Kenya lilimpa Rais Ruto asilimia 87 ya kura zao katika uchaguzi mkuu wa 2022 na kuchangia asilimia 47 ya ushindi wake dhidi ya mpinzani wake wa karibu Bw Raila Odinga.

Washirika wa Ndindi Nyoro walizindua Alhamisi, Januari 11, 2024 harakati za kumwondoa Gachagua kutoka hesabu ya Ikulu 2032, kabla ya kubadilisha ngoma Jumamosi na kumtaka Rais Ruto amteme 2027.

Wakiwa Mjini Murang’a kuzindua ruzuku kwa elimu ya shule za Sekondari za Kiharu, zaidi ya wabunge 15 kutoka maeneo mbalimbali ya nchi walisema kwamba Nyoro ndiye kesho ya urais.

Msimamo huo ulikuwa wa pili baada ya mwingine wa Februari 15, 2023 katika eneobunge la Kiharu wabunge 20 wakiwemo Seneta wa Nandi Bw Samson Cheraregei, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Nandi Bi Cynthia Muge, Mbunge wa Kimilili Bw Didmus Barasa na wengine kutoka Mlima Kenya walimtangaza Nyoro kama chaguo la wengi kumrithi Rais Ruto.

Ni hali ambayo ilirejelewa tena ambapo Alhamisi iliyopita wabunge Josses Lelmengit (Emgwen), Jematiah Sergon (Baringo), Shurie Omar (Balambala), Fred Ikana wa Shinyalu, Doris Donya kutoka Kisii na Paul Biego wa Chesumei walijiunga na wengine kutoka Mlima Kenya kumtawaza Bw Nyoro.

“Hata wanasiasa kutoka nje ya Mlima Kenya wametambua kwamba hatuna kiongozi hapa Mlima Kenya na ndio sababu wanaungana nasi kumtangaza Nyoro kama kinara wetu na tegemeo la baadaye kama mwaniaji wetu wa urais,” akasema mbunge wa Gatundu Kaskazini Bw Elijah Kururia.

Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu alirejelea mjadala huo Jumamosi, akionya kwamba Gachagua hafai kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto 2027 akisaka awamu ya pili mamlakani.

“Ukiwania urais 2027 ukiandamana na Gachagua utakuwa kwa shida. Ni afadhali umchukue Bw Nyoro ambaye hana lugha ya kudunisha wengine na kudharau viongozi wenzake,” akasema.

Mbunge wa Gatanga Bw Edward Muriu alimuunga mkono Seneta Nyutu akisema kwamba “2027 ni wakati wa Nyoro kuwa mgombea mwenza wa kumpiga teke Gachagua”.

Hata hivyo, Bw Gachagua akihutubu katika Kaunti ya Nakuru Jumamosi aliteta kuhusu spidi hatari ya wanasiasa wachanga.

Alimsihi Bw Nyoro na washirika wake wakome mbio za kumwangusha na badala yake wampe nafasi ya kumaliza mihula yake miwili mamlakani.

Akihutubu kwa lugha yake ya mama ya Gikuyu, Gachagua alilia kwamba “ithui na President tutiri andu akigu. Niturabanga anake niundu wa ruciu rwitu. Ruru rutari Njau nikuhuka ruhukaga. No nao nonginga mathii kahora matigateng’ere muno mambe mareke turikie“.

Ikitafsiriwa, ina maana kwamba “Mimi na Rais Ruto sio wapumbavu, tunajipanga kuhusu kesho yetu tukifahamu kwamba utajiri wa mifugo usio na ndama hautastawi. Lakini ni sharti hao vijana wakome mbio na watupe muda kwanza tumalize awamu yetu”.

Huku hayo yakijiri, siasa za Mlima Kenya zimepasuka kwa mirengo zaidi ya 10 hali ambayo inatishia udhabiti wa serikali ya Ruto na pia malengo ya kuwania awamu ya pili 2027.

 

[email protected]